Friday, February 1, 2013

KIWANGO CHA KUTUMA FEDHA AFRIKA CHAPUNGUZWA...

Benki ya Dunia imesema kupunguza kiwango cha kutuma fedha katika nchi za Afrika kwa asilimia tano kutoka asilimia 12.4 ya sasa, kutasaidia kuwepo zaidi ya Dola za Marekani bilioni nne kwa ajili ya wahamiaji wa bara hilo ambao ndio wategemezi wakuu wa fedha hizo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa Uhusiano wa benki hiyo nchini, Rosalia Ferrao, wakazi wa Afrika wanaofanya kazi nje ya bara hilo, ambao walituma Dola za Marekani bilioni 60 katika nchi zao kwa mwaka 2012, hulipa fedha zaidi kuliko kundi lolote la wahamiaji.
Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia katika eneo la kutuma fedha Afrika, nchi za Jangwa la Sahara ndio zenye gharama kubwa kutuma fedha ambapo kwa mwaka 2012, gharama hizo zimefikia asilimia 12.4.
“Wastani wa kutuma fedha Afrika unafikia takribani asilimai 12 juu zaidi ya wastani wa kutuma fedha popote duniani ambao ni asilimia 8.96 na ni mara mbili zaidi ya gharama za kutuma fedha katika nchi za Asia ambazo ni wastani wa asilimia 6.54,” alisema Ferrao.
Nchi za G8 na G20 zilianzisha asilimia tano kama wastani wa tozo za kutuma fedha ambazo zinatarajiwa kudumu hadi ifikapo mwaka 2015. “Gharama za juu za kutuma fedha zinaathiri kwa kiasi kikubwa mamilioni ya Waafrika,” alikaririwa Mkurugenzi wa Benki ya Dunia Afrika.
Alisema fedha itakayopunguzwa katika gharama hizo za malipo itasaidia nchi hizo za Afrika kushughulikia mahitaji muhimu ikiwemo kuwekeza kwa ajili ya maisha ya baadaye.
“Hivyo kushusha gharama hizi za kutuma fedha kutasaidia kukabiliana na umasikini Afrika,” alisema.
Alitaja baadhi ya Mataifa ya Afrika yaliyoweka gharama kubwa za kutuma fedha inayofikia wastani wa asilimia 20.7, 19.7 hadi 19.0 kuwa ni pamoja na Afrika Kusini, Tanzania na Ghana.

No comments: