Sunday, February 3, 2013

ABIRIA SABA WASAKWA AJALI YA BOTI NUNGWI...

Balozi Seif Ali Iddi.
Watu saba hawajulikani walipo kutokana na ajali ya jahazi la Sunrise lililozama katika mkondo wa Nungwi, Zanzibar.
Katika hatua nyingine, wamiliki wa vyombo vya usafiri baharini yakiwemo majahazi wametakiwa kuchukua tahadhari kabla ya kuanza  safari, ikiwa ni pamoja na kujua hali ya hewa ilivyo zaidi katika kipindi hiki cha kuvuma kwa kasi ya upepo wa Kusi.
Hayo yalisemwa na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi wakati alipowatembelea majeruhi wa ajali ya jahazi ya Sunrise katika Hospitali ya Kivunge mkoa wa Kusini Unguja.
Balozi Iddi alisema kwa mujibu wa orodha ya wasafiri na taarifa za nahodha watu 7 hawajulikani walipo kwa sasa na juhudi za kuwatafuta zinafanywa.
Watu hao ni  wanaume wawili, wanawake wawili na watoto watatu wenye umri wa  chini ya miaka 12.
“Tumeanza kazi za kuwatafuta watu waliopotea katika ajali hiyo kwa kuwashirikisha
wapiga mbizi katika hoteli za kitalii zilizopo Nungwi,” alisema.
Katika hatua nyingine, aliwataka manahodha kuchukua tahadhari kabla ya kuanza safari za baharini kwa kujua hali ya hewa na mazingira ya upepo katika eneo la Mkondo wa Nungwi.
“Taarifa tulizonazo hivi sasa kuna upepo wa Kusi ambao umekuwa ukivuma kwa kasi na hivyo kutishia usalama wa wasafiri wa vyombo vya baharini,” alisema.
Balozi, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa aliwapa pole wananchi wote waliopata ajali katika jahazi hilo.
Nahodha wa jahazi ya Sunrise yenye nambari za usajili Z 865 Abdalla Saleh pamoja na abiria Ali Juma Jabu ambao walikuwa  wamelazwa katika Hospitali ya Kivunge
wakipatiwa matibabu zaidi tayari wameruhusiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ahmada Khamis alisema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vikundi vya waokozi  wapiga mbizi wapo katika harakati za kutafuta watu waliopotea katika eneo la Nungwi.
Jahazi la Sunrise lenye uwezo wa kubeba abiria 50, lilichukua abiria 32 pamoja na mizigo ikiwemo magunia 30 ya mkaa pamoja na mbao na vitanda.
Kwa mujibu wa Kamanda Ahmada watu 25 waliokolewa katika ajali hiyo akiwemo nahodha Abdalla Saleh.
Hii ni ajali ya pili  kutokea katika Mkondo wa Nungwi. Imetanguliwa na ajali ya  mv Spice
Islander ambayo ilikuwa ikitoka Unguja kwenda Pemba na ilipata ajali wakati ilipokuwa ikikata mkondo huo.
Mkondo wa Nungwi unafananishwa na mkondo uliopo Afrika Kusini kwa kuwa na maji yenye kasi yanayosongana na kuwa tishio kwa vyombo vinavyopita eneo hilo, zaidi wakati bahari inapochafuka.

No comments: