Wednesday, January 2, 2013

MSANII WA FILAMU SAJUKI AFARIKI DUNIA...


  

Habari zilizotufikia hivi punde zinasema kwamba msanii maarufu wa filamu nchini, Juma Kilowoko maarufu kama Sajuki amefariki dunia asubuhi ya leo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Kwa mujibu wa mmoja wa ndugu wa karibu wa marehemu akiongea kwa njia ya simu, amesema Sajuki alifariki Saa 12:45 asubuhi ya leo baada ya kuwa amelazwa hospitalini hapo kwa takribani siku kumi akisumbuliwa na matatizo kadhaa ikiwamo figo zake kushindwa kufanya kazi.
Sajuki, ambaye amemuoa msanii mwenzake Wastara Juma, afya yake haikuwa ya kuridhisha kwa kipindi kirefu mwaka huu ambapo miezi kadhaa iliyopita alilazimika kuchangiwa fedha na wadau kwa ajili ya kwenda kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Appolo nchini India ambapo alifanikiwa na hali yake kutengemaa kidogo.
Baada ya takribani mwezi mmoja baada ya kurejea, hali ya msanii huyo ilibadilika tena na hivyo kulazimika kusaka fedha ili aweze kurejea tena nchini India ambapo katika siku za hivi karibuni alikuwa katika ziara ya kuchangisha fedha mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.
Katika moja ya maonesho yake, Sajuki alishindwa kustahimili kusimama jukwaani na kujikuta akianguka kabla ya kuondolewa na wasanii wenzake na kupumzishwa pembeni kwa muda.
Taarifa zaidi za kifo cha msanii huyo utazipata hapa hapa baada ya muda mfupi. MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU MAHALI PEMA PEPONI, AMEN.

No comments: