Thursday, January 3, 2013

MAASKOFU WAWILI WAJITOSA KUOKOA JAHAZI KKKT...

Askofu Mkuu Thomas Laizer.
Wakati mgogoro ukiendelea ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati, Askofu Mkuu wa dayosisi hiyo, Dk Thomas Laizer amekasimu madaraka yake kwa Askofu Msaidizi Solomoni Massangwa.
Taarifa zilizotufikia jana kutoka kwenye kikao cha viongozi wa dayosisi hiyo cha kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo, zilieleza kuwa iliamuliwa Askofu Laizer akasimu madaraka yake kwa Askofu Massangwa.
Mbali ya kuhudhuriwa na viongozi wa dayosisi na wachungaji, kikao hicho cha hivi karibuni pia kilihudhuriwa na wachungaji wastaafu na mwanasiasa maarufu ambaye ni muumini wa madhehebu hayo (jina linahifadhiwa).
Mgogoro huo uliibuka baada ya waumini kupewa waraka wa Askofu wakitakiwa kila mmoja achangie Sh 20,000 ili kunusuru mali za Kanisa zilizo hatarini kufilisiwa baada ya hoteli ya Corridor Springs kudaiwa Sh bilioni 11 na benki moja nchini.
Baada ya waraka huo, baadhi ya waumini akiwamo Mchungaji Philemon Mollel aliyekuwa kiongozi wa Usharika wa Ngateu, walitaka waliohusika na uzembe uliosababisha deni hilo, wawajibike kabla ya waumini kutoa mchango wao.
Waumini hao walikuwa wakimlenga Katibu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati, Israel ole Karyongi, ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Hoteli ya Corridor Springs. Mbali na Karyongi, pia walitaka bodi husika na menejimenti nzima kuwajibika.
Hata hivyo, hatua pekee iliyochukuliwa na kuthibitishwa na Karyongi ni kufukuzwa kwa Meneja wa hoteli hiyo, John Njoroge, ili kupisha uchunguzi wa chanzo cha kulimbikizwa kwa deni hilo.
Mtoa habari wetu akielezea sababu za Askofu Laizer kutakiwa kukaimisha madaraka yake, alisema ni kutokana na hali ya afya yake kutokuwa nzuri kwa sasa.
Askofu Laizer amekuwa akilazwa mara kwa mara katika hospitali ya rufaa ya Selian inayomilikiwa na KKKT akisumbuliwa na maradhi ambayo hayajawekwa wazi.
Hata hivyo, mtoa habari alisema Askofu Massangwa pamoja na kukasimiwa madaraka, hatashiriki shughuli za kitaifa iwapo zitajitokeza na badala yake shughuli hizo zitafanywa na Askofu Paul Akyoo wa Dayosisi ya Meru.
Kuhusu hatima ya Usharika wa Ngateu ambao mchungaji wake alisimamishwa kazi katika mgogoro huo na akaunti yake kufungwa, mtoa habari alisema akaunti ya Usharika huo iliyoko kwenye benki ya NBC iliyoamuliwa kufungwa na Karyongi imefunguliwa.
Kufunguliwa kwa akaunti hiyo kulithibitishwa na kiongozi wa Usharika huo, Rafael Kwayu aliyeeleza kuwa Mchungaji aliyesimamishwa kazi, Philemon Mollel, ameondolewa katika orodha ya watu watatu waliokuwa wameruhusiwa kusaini hundi za Usharika.
“Tumefunguliwa akaunti yetu ya Usharika, lakini Mollel ameondolewa na nafasi yake imechukuliwa na Askofu Lekashu wa Arusha Magharibi,” alisema Kwayu.
Hata hivyo, Karyongi mbali ya kutakiwa kujiuzulu kwa kuwa yeye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Corridor Springs hakuwa amefanya hivyo hadi jana, ingawa bado anashinikizwa.
Mgogoro huo unaendelea huku waumini zaidi ya 600,000 wakitakiwa kuchangia kuokoa mali za Kanisa zilizowekwa rehani ikiwamo hoteli hiyo ili zisipigwe mnada baada ya kuchelewa kulipa deni la Sh bilioni 11 za ujenzi wa hoteli hiyo.

No comments: