Friday, January 4, 2013

IDDI SIMBA AKIRI KUINGIZIWA BENKI SHILINGI MILIONI 320...

Iddi Simba.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), Iddi Simba, amekiri kuingiziwa Sh milioni 320 katika akaunti yake kutoka kampuni ya Simon Group na kudai kuwa hazikuwa kwaajili ya malipo ya awali ya mauzo ya hisa za shirika hilo.
Simba ambaye alikuwa Waziri wa zamani wa Viwanda na Biashara alidai hayo wakati akisomewa maelezo ya awali katika  kesi ya kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kulisababishia shirika hilo hasara ya Sh  bilioni 2.4.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ambao walisomewa maelezo ya awali na Wakili wa Serikali, Awamu Mbagwa ni Meneja Mkuu wa shirika hilo, Victor Milanzi na Mkurugenzi wa shirika hilo, Salum Mwaking’inda.
Simba alikiri kupokea fedha hizo na kudai hazikuhusu   masuala ya Kampuni ya Uda lakini hakutaka kufafanua zaidi zilitoka wapi na alizutumiaje.
“Si sahihi ni uzushi na uongo kuwa Sh milioni 320 zilizoingizwa kwenye akaunti yangu zilikuwa  kwa ajili ya malipo ya awali ya aina yeyote ya ununuzi wa hisa za Uda,” alisisistiza Simba
Alikiri kuwa Uda ilikuwa  na hisa milioni 15 na Serikali ilikuwa inamiliki asilimia 49 ya hisa, pia waliuza hisa hizo kwa kampuni ya Simon Group kwa kufuata utaratibu na kuwa uamuzi wa kuuzwa kwa hisa hizo siyo wake bali ni wa Bodi ya Wakurugenzi wa Uda.
Awali Wakili Mbagwa alidai kuwa Agosti 2009 Mkurugenzi wa Kampuni ya Simon Group aliwasilisha barua ya kutaka kununua hisa za kampuni hiyo na washitakiwa kupitia barua iliyotolewa Septemba 2 mwaka 2009 na kusainiwa na Milanzi, waliiitaka kampuni hiyo kulipa malipo ya awali ya Sh milioni 400 kwenye akaunti namba 0210001002 inayomilikiwa na Simba.
Septemba 3, 2009 Kampuni hiyo ilituma Sh milioni 250 kwenda kwenye akaunti ya Simba iliyopo kwenye Benki ya M tawi la Sea View, ambapo fedha zilipoingia kwenye akaunti hiyo Simba anadaiwa alitoa Sh milioni 100 kwenda akaunti ya Africarriers kama malipo ya ununuzi wa gari aina ya Toyota Land cruiser VX yenye namba za usajili T 561 BCX.
Hata hivyo Simba alikana kutoa fedha hizo kwa ajili ya kununua gari pia alikana kuwa kabla ya fedha hizo kutumwa akaunti yake ilikuwa na Sh milioni tatu kama upande wa mashitaka ulivyodai.
Kwa upande wake Milanzi alikana kutumia madaraka yake vibaya katika kuuza hisa za uda kinyume cha utaratibu wa manunuzi na kukiri alisaini barua ya maelekezo ya malipo iliyoidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Ilvini Mugeta aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 4 na 5 mwaka huu kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa.
Inadaiwa Septemba 2, 2009 jijini Dar es Salaam, Simba na Milanzi walikula njama ya kuchepusha fedha na   kughushi barua wakionesha kuwepo kwa kiwango zaidi cha fedha kwenye akaunti zote za UDA Ltd.
Aidha wanadaiwa walichepusha Sh milioni 320 wakijifanya ni malipo ya awali ya mauzo ya hisa katika shirika hilo fedha ambazo walijipatia kutokana na nyadhifa zao.
Inadaiwa Simba na Mwaking’inda wakati wakitekeleza majukumu yao, kwa makusudi walitumia vibaya nafasi zao wakaharibu hisa milioni 7.8 zisizotumika za UDA,   Shirika linalomilikiwa kati ya Serikali na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

No comments: