Saturday, January 5, 2013

AMUUA MKEWE KWA PANGA AKIDAI NI MSHIRIKINA...

Kamanda Diwani Athumani.
Lena Mbughi, mwanamke mwenye umri wa miaka 34, ni miongoni mwa Watanzania waliouona mwaka mpya wa 2013 na bila shaka alikuwa na matumaini ya kuumaliza mwaka huu, na pengine kuishi hadi kupata wajukuu.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Diwani Athumani, juzi Alhamisi (Januari 3), ilimkuta mwanamke huyo ambaye bado kijana, akiwa buheri wa afya na hakujua kama hiyo ilikuwa ni siku yake ya mwisho duniani na kwamba kifo chake kingekuwa cha kinyama, tena kikitokana na mumewe mpenzi, Israel Kayuni.
Kamanda Athumani anasimulia kwamba Alhamisi hiyo tulivu, saa 8:00 mchana, Lena, aliamua kujipumzisha kwenye mkeka chumbani kwake, pale katika kitongoji cha Sambandolo, kijijini Ipapa, Kata ya Ipunga wilayani Mbozi.
Anasema wakati Lena akiwa kajipumzisha akisaka usingizi wa mchana baada ya kula chakula, mumewe huyo, Israel (jina kama la malaika anayeaminiwa kutoa roho kwa imani ya baadhi ya dini) aliingia pale chumbani na panga, akamvamia mkewe na kumkata nalo na kusababisha kifo chake.
Kamanda Athumani anasimulia zaidi kwamba baada ya mauaji hayo, Israel alikimbia na mpaka tunakwenda mitamboni alikuwa hajulikani alikokimbilia licha ya kutafutwa sana.
Anasema polisi ambao wameahidi kumsaka kwa udi na uvumba muuaji huyo,   walipofika eneo la tukio baada ya kupewa taarifa walikuta mwili wa Lena ukiwa katika dimbwi la damu huku panga lililotumiwa na mumewe kunyofoa uhai wake likiwa pembeni.
Kinachosikitisha ni sababu za Israel kuchukua hatua hiyo, kumuua bila huruma mtu ambaye aliwahi kumnyima usingizi akihaha ili awe mkewe. Kamanda Diwani Athumani anazitaja sababu hizo kwamba ni kumtuhumu kuwa mshirikina.
“Uchunguzi wa awali unaonesha kwamba mtuhumiwa Israel Kayuni alikuwa akimtuhumu mkewe Lena kuwa anajihusisha na vitendo vya kishirikina. Walikuwa na ugomvi wa mara kwa mara kuhusu tuhuma hizi na ndiyo sababu ya kuchukua uamuzi huo usiofaa… Licha ya kudanganywa na waganga wa jadi, lakini alipaswa kutumia njia za mazungumzo na si kujichukulia sheria mikononi,” alisema Kamanda Athaman akionesha masikitiko.
Katika tukio jingine, dereva teksi aliyefahamika kwa jina la  Emmanuel Mbembela (30) mkazi wa Mtaa wa Sogea katika mji mdogo wa Tunduma wilayani Momba, amekutwa  ameuawa na watu wasiofahamika na mwili wake kutupwa kichakani ukiwa na majeraha usoni na utosini.
Kamanda Athumani alisema mwili wa Emmanuel ulikutwa Januari 2 mwaka huu saa 12:30 jioni katika kichaka kilichopo jirani na Reli ya Tazara, eneo la kijiji cha Mlowo, barabara ya Mlowo-Kamsamba.
Alisema, awali gari la dereva huyo aina ya Toyota Spacio lenye namba za usajili T 381 BMT lilikodiwa na watu wasiofahamika na ambao haikujulikana walitaka kupelekwa wapi.
Kamanda Athumani alisema jeshi hilo linaendelea kuwasaka watuhumiwa wa matukio hayo yote na kuomba raia wema walio na taarifa za mahali walipo kulisaidia jeshi hilo.

No comments: