POLISI WADAIWA KUGAWANA MILIONI 150 ZA TUKIO LA UJAMBAZI KARIAKOO...

Kamanda Suleiman Kova.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova ameteua jopo la wapelelezi kuchunguza tuhuma za askari Polisi kugawana Sh milioni 150 zilizoporwa katika tukio la ujambazi lililotokea Kariakoo wiki hii.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda Kova alisema ameamua kuunda Tume hiyo kutokana na taarifa zilizojitokeza katika baadhi ya vyombo vya habari kuwa baada ya uporaji huo Desemba 18, mwaka huu, askari walichukua fedha zile na kugawana.
“Jopo hili limepewa muda mfupi sana, pengine siku mbili tatu hizi mtapata majibu ya uchunguzi, wananchi wanatakiwa kuelezwa mapema ukweli wa tuhuma hizo kwa hiyo kazi itafanyika usiku na mchana,” alisema Kamanda Kova.
Tukio hilo la ujambazi lilitokea katika Mtaa wa Mahiwa na Livingstone katika eneo la Kariakoo ambapo majambazi wakiwa katika pikipiki, walipora fedha hizo na kutokomea nazo, huku askari wakifanikiwa kumkamata mtuhumiwa wa ujambazi aliyekuwa na silaha bila fedha.
Alisema habari zilizoko katika vyombo hivyo vya habari zimesisitiza kwamba walikwenda kugawana fedha hizo katika Kata ya Jangwani.
Kutokana na taarifa hizo, Kamanda Kova alisema Polisi  imezichukua kwa uzito wa hali ya juu na kuona bora uchunguzi wa kina ufanyike ili kuthibitisha ukweli.
Kamanda Kova alisema jopo hilo ni la watu watano linaongozwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Ahmed Msangi na ikibainika kuwa tuhuma hizo ni za kweli, wale waliohusika watachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Ili kuhakikisha uchunguzi huo unafanyika kwa haraka, tunaomba mtu yeyote mwenye taarifa sahihi ajitokeze bila kusita na endapo atakuwa msiri atalindwa ili asisumbuliwe,” alisema Kamanda Kova.
Alisema wale wote waliokuwepo wakati wa kukamatwa kwa watuhumiwa wa ujambazi huo wajitokeze ili kueleza jinsi walivyoshuhudia na kubaini endapo askari waliokuwepo waliondoka na ‘fuko’.
Pia aliomba wananchi walioshuhudia askari hao wakiwa Jangwani wanakodaiwa kwenda na pia nyumba waliyotumia kugawana.
Katika uporaji huo, mtuhumiwa wa ujambazi, Augustino Kayula (24) alifariki dunia akiwa chini ya ulinzi wa Polisi na katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu.
Katika tukio hilo, inadaiwa kwamba Kayula na wenzake wawili wakiwa wamepanda pikipiki mtindo wa mshikaki, walivamia duka la Kampuni ya Artan Ltd na kupora Sh milioni 150, zilizokuwa zikitolewa dukani eneo la Kariakoo kwenda benki.
Kova pia alisema Polisi imekamata pikipiki 77 kwa makosa mbalimbali ya barabarani ikiwemo matukio ya ujambazi kwa sasa wanatumia usafiri huo kwa sababu ni rahisi kupenya barabarani kwa urahisi.

No comments: