HALI BADO TETE KKKT, WAJUMBE WASUSIA CHAKULA KIKAONI...

Kanisa la KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati.
Hali ni tete ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, baada ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Dayosisi kilichoitishwa kujadili madeni makubwa yanayoikabili Dayosisi hiyo, kusambaratika juzi.
Kuvunjika kwa kikao hicho kilichoitishwa kwa dharura, kulitokana na wajumbe wa kikao hicho kugawanyika pande mbili kutokana na tofauti za misimamo ya wajumbe.
Mgawanyiko huo umetokana na upande mmoja kutaka Bodi ya Hoteli ya Corridor Springs chini ya Uenyekiti wa Katibu wa Dayosisi, Israel ole Karyongi kuwajibika huku upande mwingine ukipinga hoja hiyo.
Hoteli hiyo inayomilikiwa na Dayosisi hiyo iko hatarini kupigwa mnada baada ya kushindwa kulipa marejesho ya mkopo uliochukuliwa kutoka benki moja ya biashara ili kuijenga mwaka 2006.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho kilichofanyika katika hoteli hiyo, zinasema kulitokea mabishano miongoni mwa wajumbe na mwishowe kikao kilimalizika bila kufuata utaratibu wa kawaida wa mikutano unaohusisha sala ya kufungia. 
“Mwandishi hali ni mbaya, kulikuwa na mabishano makali upande mmoja ukitaka Bodi ya Hoteli iwajibishwe wakiwa na hoja na wengine wakipinga bila hoja…kila mjumbe aliamua kuondoka ukumbini bila kuaga wala kufikia msimamo wowote,” alisema mtoa habari wetu ambaye ni mjumbe wa kikao hicho.
Alisema mabishano na malumbano hayo, yalisababisha chakula kilichoandaliwa kwa ajili ya wajumbe hao kisuswe huku baadhi ya wajumbe wakiamua kununiana.  
“Imefikia mahali wajumbe hata kusalimiana hawataki kutokana na tofauti zao, lakini inabidi kusali sana kuiombea Dayosisi yetu isisambaratike kwani watu wanatetea ufisadi wakati wengine wanataka viongozi wa kanisa hilo wawajibike kwa uzembe huo,” aliongeza mjumbe mwingine ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini.
Karyongi alipopigiwa simu jana alikataa kata kata kuzungumzia yaliyojiri katika kikao hicho akidai kuwa yupo safarini na atafuwe Jumatatu ijayo ili kutoa ufafanuzi kama ikibidi.
Hali ya sintofahamu katika Dayosisi hiyo imetokea baada ya waumini wake kutakiwa kuchangia Sh 20,000 kila mmoja, ili kulipa deni la benki hiyo ya biashara kabla ya Desemba 31, mwaka huu ili kunusuru mali za
Dayosisi hiyo ikiwamo Hoteli ya Corridor Springs na Hospitali ya Rufaa ya Selian zisipigwe mnada.
Chanzo cha mgogoro huo ni maagizo mawili tofauti ya kuwataka waumini hao wachangie kunusuru mali za Dayosisi hiyo yaliyotolewa ndani ya mwezi mmoja uliopita.
Katika maagizo ya kwanza yaliyotolewa kwa wakuu wa majimbo wa Dayosisi katika kikao kilichoketi Novemba 27, mwaka huu, ilielezwa kuwa deni lilikuwa Sh milioni 680.
Habari za uhakika zilisema kuwa kikao hicho kiliamua kila jimbo lichangie fedha kwa kadiri ya uwezo wa waumini wake na kila moja lilipangiwa kiasi wanachotakiwa kuchanga ili kuokoa mali za Dayosisi.
Kwa mfano moja tu katika makadirio hayo, Jimbo la Arusha Magharibi lilitakiwa kuchangia Sh milioni 300 kabla ya mwishoni mwa Machi mwakani.
Vyanzo vya habari vilisema kuwa maagizo hayo yalitolewa kwa wakuu wa majimbo sita yanayounda Dayosisi hiyo ya Kaskazini Kati.
Hata hivyo, wakati maagizo hayo yakitekelezwa, Desemba 9, mwaka huu Makao Makuu ya Dayosisi ilitoa waraka wa kutaka kila muumini kuchangia Sh 20,000 kama kiwango cha chini kabla ya Desemba 31, mwaka huu.
Hatua hiyo ilidaiwa kuwa na lengo la kunusuru mali za Dayosisi hiyo hasa Hoteli ya Corridor Springs inayodaiwa na benki kiasi kinachofikia Sh bilioni 11 kutokana na malimbikizo ya mkopo.
Hata hivyo, Karyongi hivi karibuni alilieleza gazeti hili kuwa deni hilo si Sh bilioni 11 kama inavyodaiwa bali ni Sh bilioni moja ingawa kwa waraka wa kuwataka waumini zaidi ya 600,000 kuchangia Sh 20,000 kila mmoja, wangepata Sh bilioni 12.
Aidha, taarifa zilizolifikia gazeti hili zilibainisha kuwa Askofu Mkuu wa KKKT, Dk Alex Malasusa amewasili jijini Arusha, na inaelezwa kuwa mgogoro huo ni mojawapo ya sababu ya kuwapo hapa.

No comments: