MFANYABIASHARA APORWA MILIONI 50 ARUSHA...

Kamanda Liberatus Sabas.
Majambazi wanne wakiwa na bastola na bunduki, juzi walimpora mfanyabiashara wa Kiasia zaidi ya Sh milioni 50 katika kituo cha mafuta cha Five Star kilichopo karibu na jengo la Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC) jijini Arusha.
Kwa mujibu wa walioshuhudia tukio hilo, majambazi hao wakiwa na usafiri wa pikipiki maarufu kwa jina la bodaboda, walimfuatilia mfanyabiashara huyo ambaye jina lake halikupatikana mara moja, kutoka PPF.
Habari zilisema mbali ya kutoka katika shirika hilo, pia mfanyabiashara huyo alipitia benki kwa ajili ya kuchukua malipo ya mishahara ya wafanyakazi wake.
Mtoa habari ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini, alidai kuwa katika mizunguko ya mfanyabiashara huyo, majambazi hao walikuwa wakimfuatia na usafiri huo kila alikokwenda na kutoka.
Vyanzo vya habari vilidai baada ya mfanyabiashara huyo kumaliza shughuli za uchukuaji fedha, alielekea ofisini kwake eneo la viwanda la Unga Ltd na ndipo alipogundua anafuatiliwa na watu ambao alihisi kuwa si watu wema.
Inadaiwa alipoona hivyo, aliamua kukimbilia katika kituo cha mafuta cha Five Star, lakini jitihada hizo hazikumsaidia kwani zilipigwa risasi mbili hewani na gari yake kuvamiwa na kuchukuliwa fedha.
Majambazi walipiga risasi tatu hewani kwa lengo la kutawanya watu na baada ya kufanikiwa hilo, pia walipiga risasi kioo cha gari na kumvamia akiwa ndani ya gari na kuchukua furushi la fedha na kutokomea.
Hata hivyo, shuhuda wetu alisema iwapo polisi wangefanikiwa kuwahi eneo la tukio, majambazi hao wangekamatwa kwani pikipiki waliyokuwa wakitumia, iligoma kuwaka kwa muda wa dakika 15, lakini walipofanikiwa kuwasha waliondoka kwa kasi kubwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabasi alipotafutwa kwa njia ya simu jana, alisema hana taarifa juu ya tukio hilo na aliomba muda kulifuatia.
“Kwa sasa sina taarifa juu ya tukio hilo, lakini hebu nipe muda nimuulize Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa halafu ntakupa taarifa rasmi,” alisema Kamanda Sabas alipoulizwa jana.

No comments: