![]() |
| Stephen Wassira. |
Majigambo ya Mbunge wa Jimbo la Bunda, Stephen Wassira (CCM) ambaye pia ni Waziri katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, yamewachefua viongozi wa Chadema kiasi cha kuamua kupeleka makamanda wake jimboni kwa lengo la kupiga kambi ya wiki moja ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuhakikisha harudi madarakani mwaka 2015.
Wassira, mmoja wa wanasiasa wakongwe na wenye kuheshimika, hivi karibuni aliwabeza Chadema akisema yeye ndiye mwarobaini wa chama hicho.
Uamuzi wa kuweka kambi inayotajwa kuwa ya nyumba kwa nyumba, kijiji kwa kijiji na kata hadi kata ndani ya Bunda, umethibitishwa na Mratibu wa kampeni iliyopewa kaulimbiu ya `Ondoa CCM na Wassira Bunda’, Lucas Webiro.
Alisema kuwa, kuanzia leo watakuwa na kazi moja ya kutaka `kumwanika’ Wassira na kwamba kumwacha aendelee kutamba ni sawa na kumwogopa na kumpa sifa walizodai hana.
“Wasira alijigamba kwamba ni mwarobaini wa Chadema. Sasa tunataka tummalize yeye na chama chake kuanzia hapahapa nyumbani kwake. Tunajua mapungufu yake…tutawaambia WanaBunda,” alisema Webiro.
Kuhusu makamanda wa chama hicho, Webiro ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chadema, alisema itakuwa na wabunge wanane, akiwemo pia aliyesimamishwa, Godbless Lema wa Arusha Mjini.
Wassira, wakati akiomba kuchaguliwa nafasi ya ujumbe wa NEC ndani ya CCM mjini Dodoma mwezi uliopita, aliwataka wajumbe wa mkutano mkuu kwa kumwamini kwa kuwa yeye ndiye mwarobaini wa chama kikuu cha upinzani kwa sasa nchini, Chadema.
.jpg)
No comments:
Post a Comment