CCM YAMSHUKIA MAALIM SEIF KWA KUPOTOSHA MAONI YA KATIBA...

Maalim Seif Shariff Hamad.
Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kimemtaka Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, kuacha kuwavuruga na kuwayumbisha Wazanzibari katika mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya Katiba baada ya kutoa takwimu za uongo kwamba asilimia 66 ya waliotoa maoni wanataka Muungano wa Mkataba.
Akizungumza ofisini kwake Kisiwandui mjini Unguja, Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM Zanzibar, Waride Bakari Jabu, alisema Maalim Seif hana mamlaka kwa mujibu wa sheria kuilazimisha Tume ya Rais ifuate na kutii matakwa ya chama chake.
“CCM ndiyo tuliyofungua milango ya maridhiano ya kisiasa ambapo nia yetu ni kuondokana na siasa za chuki na uhasama ambazo zilirudisha nyuma maendeleo yetu,” alisema Jabu.
Alisema kitendo cha viongozi wa CUF kutoa takwimu kwenye majukwaa ya kisiasa ni ukiukwaji wa sheria na lengo lake si jema.
Alisema kwa sasa bado vyama vya siasa pamoja na wananchi wanaendelea na mchakato wa kutoa maoni ya Katiba, kwa hivyo sio busara hata kidogo kwa viongozi wa CUF kutoa takwimu hizo ambazo sio sahihi.
“Chama Cha Mapinduzi kinajiuliza hawa viongozi wa CUF takwimu za maoni ya Katiba wamezipata wapi? Kwa sababu mchakato huu kwa mujibu wa sheria unaratibiwa na Tume ya Rais ya Kukusanya Maoni ya Katiba,” alisema Jabu na kushangazwa na CUF kutoa takwimu hizo.
Aidha, CCM imemshauri Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kutumia fursa aliyonayo kumshauri vizuri Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein masuala ya kisiasa na sio kutumia majukwa ya kisiasa vibaya.
CUF mwishoni mwa wiki kilifanya mkutano wa hadhara na kuhutubiwa na Katibu Mkuu wake, Maalim Seif ambapo yeye na viongozi wengine, walitoa takwimu kuhusu maoni ya Katiba na kusema kwamba asilimia 66 ya wananchi wa Zanzibar wanataka muundo wa Muungano wa Mkataba.

No comments: