WANAFUNZI WANAOFANYA UKAHABA CHUO KIKUU DODOMA WAANZA KUSAKWA...

Moja ya majengo ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Dodoma (UDOSO), imeanza uchunguzi ili kubaini wanafunzi wa chuo hicho wanaojihusisha na biashara ya ngono.
Viongozi hao wamefikia hatua hiyo baada ya taarifa iliyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari wiki iliyopita, kuwa baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakijiuza mitaani hasa usiku.
Akizungumza na waandishi wa habari jana chuoni hapo, kwa niaba ya wanafunzi hao, Rais wa Udoso, Yunge Paul alisema tayari kazi ya kuchunguza imeanza na watakaobainika watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Alisema kama kweli vitendo hivyo vinafanyika, wanafunzi hao wanashusha heshima ya chuo hicho ambacho kina wasomi wengi na kinapaswa kuwa kioo cha jamii.
Yunge alisema taarifa hiyo ya kashfa ya ngono iliyoripotiwa na vyombo vya habari imesononesha nchi nzima, ukiwamo uongozi wa chuo, wazazi na wanafunzi.
Hata hivyo, alisema taarifa hiyo haikutoa uzito na ushahidi wa kutosha kuwa wanafunzi wa chuo hicho wanajiuza na wamekuwa wakionekana sehemu mbalimbali za starehe mjini hapa.
Alivitaka vyombo vya habari  vilivyotoa taarifa hiyo virekebishe kauli kama havina ushahidi ili kurudisha heshima na imani kwa Chuo Kikuu cha Dodoma.
Alisema wakati taarifa hiyo inatolewa katika vyombo vya habari Dodoma ilikuwa na watu wengi na inawezekana walioonekana kufanya vitendo hivyo si wanafunzi kwani hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaothibitisha kuwa wanafunzi wa UDOM wanajiuza.
Paul alisema mwanafunzi wa UDOM anajulikana kwa kitambulisho chake na inawezekana mtu yeyote akajitambulisha kutoka chuo hicho.
“Kama ushahidi wa wanafunzi wanaojiuza upo, basi   upelekwe chuoni hapo ili wahusika wachukuliwe hatua za kinidhamu,” alisema.

No comments: