MAELFU WAJITOKEZA KUMZIKA SHARO MILIONEA KIJIJINI KWAKE...

Maelfu ya mashabiki wakiwa wamekusanyika katika mazishi ya msanii Sharo Milionea kijiji kwao Lusanga, wilayani Muheza, Tanga jana. PICHA NDOGO: Mwili wa Sharo Milionea ukiwa umewekwa tayari kwa ajili ya maziko.
Maelfu ya wakazi, mashabiki na wasanii wa muziki na filamu nchini wamejitokeza kwa wingi kumzika msanii, Hussein Mkieti ‘Sharo Milionea’ kijijini kwao Lusanga, Muheza.
Sharo Milionea alizikwa jana mchana na kuhudhuriwa na maelfu ya watu kutoka mikoa mbalimbali nchini, akiwamo mjumbe wa Bodi ya Shirikisho la Filamu nchini, Nape Nnauye.
Naye Rais Jakaya Kikwete alielezea masikitiko yake na kutuma salamu za rambirambi kwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara.
Wasanii hao ni mwigizaji wa kundi la Kaole,  Khalid Mohamed ‘Mlopelo’ aliyefariki dunia Novemba 22 kutokana na maradhi yaliyokuwa yanamsumbua kwa muda mrefu.
Pia msanii wa filamu, John Maganga aliyefariki dunia Novemba 24, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa matibabu. 
Vilevile usiku wa Novemba 27 msanii mwingine maarufu wa futuhi na muziki wa kizazi kipya, Hussein Mkieti ‘Sharo Milionea’ alikufa kwa ajali ya gari alilokuwa akiendesha.
Gari hilo lipinduka katika maeneo ya Maguzoni Songa, wilayani Muheza mkoani Tanga, Mkieti akiwa njiani kwenda nyumbani kwao katika kijiji cha Lusanga, Muheza.
“Nimeshtushwa na kuhuzunishwa mno kutokana na taarifa za vifo vya wasanii hawa ambao kwa hakika mchango wao mkubwa katika tasnia ya muziki na maigizo nchini ulikuwa unatambuliwa na kuthaminiwa na wananchi wengi. Pengo waliloliacha ni kubwa na ambalo si rahisi kuzibika katika kipindi kifupi,” alisema Rais Kikwete katika salamu zake.
Aliongeza: “Kutokana na msiba huu mkubwa, ninakutumia wewe Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk  Fenella Mukangara, kwa kuwapoteza wasanii hawa maarufu ambao wameliletea heshima Taifa letu katika nyanja za muziki na sanaa kwa ujumla. 
“Kupitia kwako, naomba unifikishie salamu zangu za rambirambi kwa familia za marehemu wasanii wote hao ambao najua machungu waliyonayo kwa sasa ni makubwa, nami naungana nao katika kuomboleza vifo vya wapendwa wao.  Namwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza mahali pema peponi roho za marehemu, Amina”. 
Rais Kikwete aliwaomba wanafamilia wote wa marehemu wawe na moyo wa uvumilivu na ujasiri katika kipindi chote cha maombolezo ya wapendwa wao, kwani yote ni mapenzi yake Mola.
Aidha aliomba rambirambi ziwafikie wasanii wote nchini ambao, katika kipindi kifupi kilichopita, walipoteza wasanii watatu maarufu ambao enzi za uhai wao walisaidia sana kuinua kiwango cha sanaa nchini.  
Naye Dk Mukangala, alisema Serikali imepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za misiba ya wasanii hao watatu iliyotokea kwa mfululizo mwezi huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, alisema vifo vya wasanii hao vimefuatana kwa kipindi kifupi Novemba jambo ambalo limeleta simanzi kwa Serikali, wasanii wenzao na wapenzi wa tasnia za filamuna muziki nchini.
“Wasanii wote hawa ndio kwanza wameanza kung’ara katika tasnia ya filamu na sote tu mashahidi kuwa walianza kuleta matumaini makubwa katika kukuza na kuendeleza tasnia hiyo na muziki, hususani muziki wa kizazi kipya, lakini ghafla wametutoka, inasikitisha sana,” alisisitiza.
Alisema vifo hivyo ni pigo kwa Taifa na jamii nzima ya Watanzania hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali imekuwa ikifanya juhudi za kuhakikisha tasnia ya filamu na muziki zinakuwa rasmi.
“Serikali inatoa pole nyingi kwa familia, ndugu, jamaa na wote walioguswa na misiba hii. Ni imani ya Serikali kuwa wasanii wa tasnia hizi wataendeleza mazuri yaliyofanywa na wenzao na kuendelea kuwaenzi,” alisema.
Yeye alizaliwa pacha na mwenzake wa kiume pia ambaye alifariki dunia baada ya kuzaliwa lakini alitanguliwa na dada zake wawili.

No comments: