Friday, November 16, 2012

WALIMU WALALAMIKIA KUCHAPWA VIBOKO HADHARANI...

Fikiria mwalimu mbele ya wanafunzi wako unacharazwa viboko na mzazi au askari wa jeshi la jadi maarufu kama sungusungu utajisikiaje?
Hivyo ndivyo wanavyodai kufanywa baadhi ya walimu wa shule za msingi na sekondari katika wilayani   hapa. Hali hiyo inafanya washindwe kutekeleza  majukumu yao ya kutoa elimu ya darasani na ya nje ya darasa (kitabia) kwa wanafunzi wao.
Walimu hao walibainisha hali hiyo jana kartika semina ya siku tatu ya Utawala Bora na Demokrasia inayoendelea wilayani hapa ikiwa imeandaliwa na  Shirika la Kuimarisha Demokrasia na Utawala bora kwa Vijiji na Kata ( ADLG)  lenye makao makuu Mwanza, kupitia mradi wa “Chukua Hatua” wenye lengo la kuujengea uwezo umma (walimu, wakulima na viongozi wa dini) kushiriki katika masuala yanayohusu demokrasia na utawala bora kwenye maeneo yao.
Akizungumza kwa uchungu kwenye semina hiyo, Mwalimu Semua Katule wa sekondari ya Kadoto, katika kata ya Kadoto alisema amekuwa anafanya kazi katika mazingira magumu shuleni hapo, kutokana na vitendo vya kunyanyaswa na sungusungu ambao siku moja walimfuata shuleni na kumwamuru ahudhurie mkutano wao kutokana na wizi katika duka uliofanyika usiku  kijijini hapo.
“Siku hiyo nilikuwa kwenye michezo ya wilaya, ghafla nikajisikia kuumwa malaria, nikameza dawa masikio yakaziba nikarudi kwenye kituo changu cha kazi, kumbe usiku huo kuna wizi ulifanyika dukani, sungusungu walipiga mwanu usiku huo kuwataka wakazi wa kijiji kuhudhuria asubuhi mkutanoni; kesho yake asubuhi nikiwa bado nimelala nilisikia  mlango wangu ukigongwa na  nilipofungua nikakutana na   sungusungu wanane walinishika na kuniburuza kwa nguvu hadi mkutanoni,”  alisema na kuongeza:
 “Nilishangaa kuburuzwa na kufikishwa kwenye mkutano wa jadi, hakika walinidhalilisha ukizingatia kijiji kile ndiko ninakofanya kazi na kusulubiwa kwa maneno makali mbele ya wanafunzi wangu, hivi katika kuwafundisha watanitii na kuniheshimu kweli? ” Alihoji.
Aliongeza kwamba walimu wakiadhibu wanafunzi inapobainika kufanya makosa wanafunzi huungana na baadhi ya wanakijiji kuvamia walimu hao na kuwapiga.
Mwalimu Onesmo Makota wa sekondari ya Senani, alisema baadhi ya walimu hapa wamekuwa wakicharazwa viboko na viongozi wa jadi wanapochelewa mikutano yao ya jadi.
Alisema kumekuwapo uhusiano mbaya kwa baadhi ya shule za msingi na sekondari wilayani hapa na jamii, hali inayosababisha baadhi ya walimu kudharauliwa na kufikia hatua ya baadhi yao kuchapwa viboko.
“Ikitokea ajenda ya walimu ikaingizwa kwenye mikutano ya hadhara ya kijiji na ya jadi hupuuzwa  na kutokana na  uhusiano mbaya baina yetu, wananchi na viongozi wetu, hali inayosababisha wakati mwingine kuchapwa viboko,” alisema.
Mwalimu Grace Sigira wa shule ya msingi Kadoto alisema baadhi ya wanajamii Simiyu bado hawathamini umuhimu wa elimu na kuwa hata kamati za elimu za shule za msingi na sekondari zinaelimisha wakazi wa hapa umuhimu wa watoto kusoma, lakini hawaoni umuhimu huo.
“Sehemu kubwa ya wazazi wana mtazamo hasi juu ya kuwapo walimu, wao wanafikiri walimu wengi wako katika vijiji vyao kwa bahati mbaya … hawathaminiwi kama wataalamu walioajiriwa na Serikali,” alisema.
Walimu hao walisema inapofika wakati wa mitihani ya kitaifa ya kuhitimu elimu ya msingi na ya vidato vya pili na nne,  baadhi ya wazazi wilayani hapa huzuia watoto wao (hasa wasichana) wasifanye mitihani hiyo ili waozwe.
Akitoa mfano, Mwalimu Beatrice Lukiko wa sekondari ya Kulime katika tarafa ya Sengerema, alisema baadhi ya wanafunzi wa kike walizuiwa na wazazi na walezi kufanya mitihani ya Taifa ya kidato cha pili na cha nne ili waolewe.
 “Lakini pia tunakabiliana na uhaba wa walimu, kwa mfano shuleni kwangu walimu tulioajiriwa ni wawili tu, mimi, Mkuu wa Shule na mwalimu wa kujitolea, kwa shule yenye mpaka kidato cha nne, kwa waandishi wa habari mlioko hapa na wawakilishi wa CWT naomba iambieni Serikali isijaze walimu wengi mijini, walimu wa vijijini tuna mzigo mkubwa wa kufundisha  maana tuko wachache sana na hatusholezi ,” alisema Lukiko.
Mkurugenzi Mtendaji wa ADLG, Jimmy Luhende, alitaka walimu hao kutumia fursa ya taaluma na umoja wao kutafakari na kujadiliana na jamii ili kutatua changamoto wanazokutana nazo.

No comments: