Friday, November 16, 2012

MTOTO WA MIAKA MINNE ACHOMWA MOTO NA KULISHWA KINYESI MBEYA...

Mtoto huyo akiwa amelala kitandani katika Hospitali ya Rufaa mjini Mbeya baada ya kukatwa mkono.
Wadau mbalimbali jijini Mbeya wamelaani kitendo cha kinyama alichofanyiwa mtoto wa miaka 4 cha kunyanyaswa kikatili kwa kuchomwa moto na kulazimishwa kula kinyesi.
Mtoto huyo (jina limehifadhiwa) ambaye amelazwa katika Hospitali ya Rufaa jijini hapa imedaiwa amekuwa akifanyiwa vitendo mbalimbali vya kuumizwa mwili na moyo wake ikiwemo kuchomwa moto mkono wake wa kushoto na shangazi yake, Bahati Rukangara.
Katibu wa asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Mbeya Paralegal Unit (Mbepau), Jane Lawa alisema jana kuwa kitendo hicho ni cha kinyama kisichopaswa kufanywa binadamu yeyote.
Lawa alisema kuwa unyama aliotendewa mtoto huyo ulisababisha akatwe mkono wake kutokana na kuharibiwa vibaya kwa kuchomwa moto. 
Wakazi wa Mtaa wa Isangakati Kata ya Isanga, Antony Bukuku na Alex Mwasikilari walisema kwa nyakati tofauti kwamba hatua stahiki za kisheria zinapaswa kuchukuliwa haraka na vyombo vya dola dhidi ya mtuhumiwa, ili kutoa fundisho kwake na wengine.
“Si huyu tu yawezekana wapo watoto wengi wanaoteseka lakini hakuna aliyeibuka kuwatetea na huenda wanafichwa ndani kama alivyofichwa mtoto huyu. Jamii haiwezi kugundua kwa urahisi,” mlisema Mwasikirali.
Mtoto huyo alilazimika kukatwa mkono wake Novemba 13 mwaka huu na kwa mujibu wa mama yake mdogo anayemhudumia  hospitalini hapo, Silvia Salvatory  afya yake inaendelea vizuri.
Mama huyo aliwambia waandishi wa habari kuwa taarifa za awali zinaonesha shangazi huyo alianza kumtesa mtoto huyo muda mrefu mara baada ya kumchukua kutoka kwa wazazi wake wanaoishi Bukoba mkoani Kagera.
Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Thomas Isidori  alisema hali iliyosababisha mtoto huyo kukatwa  mkono ni siri kati yake na daktari aliyemhudumia  na kwamba  sheria ya uuguzi inakataza kutoa taarifa ambazo ni siri.

No comments: