SERIKALI YAIFUNGA SHULE YA SEKONDARI BAGAMOYO...



Habari zilizotufikia zinasema kuwa Serikali wilayani Bagamoyo leo imetangaza kuifunga Shule ya Sekondari Bagamoyo maarufu kama Magambani kwa muda usiojulikana kutokana na madai ya kuzuka ghasia za kidini.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, imeelezwa kwamba ulifanyika uchaguzi wa Kiongozi wa wanafunzi shuleni hapo ambapo wagombea walikuwa ni wawili, mmoja wa dini ya Kikristo na mwingine Kiislamu.
Baada ya matokeo kutangazwa na mgombea kutoka dini ya Kikristo kushinda, inadaiwa kwamba wanafunzi wa Kiislamu walipinga matokeo hayo na ndipo ghasia hizo zikazuka.
Pia kulikuwa na madai kwamba wanafunzi wa Kiislamu walipanga kuchoma moto majengo ya shule hiyo, hivyo wanafunzi wa Kikristo kutakiwa kuondoka haraka kwenye maeneo ya shule hiyo.
Lakini chanzo chetu cha habari kimesema baadhi ya wanafunzi wa shule waliohojiwa kwa nyakati tofauti wamekanusha kuwa na tofauti hizo za kidini na kusisitiza kwamba ni kampeni chafu ya baadhi ya walimu wanaopandikiza mbegu mbaya ya udini miongoni mwa wanafunzi ili kuleta mtafaruku shuleni hapo.
Wameendelea kukieleza chanzo chetu kwamba, katika siku za karibuni walimu hao wamefikia hata kuwapachika majina wanafunzi hao kama Al-Shaabab, Al-Qaeda n.k.
Baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha Sita wameelezea kusikitishwa kwao na hatua hiyo ya kuifunga shule hiyo hasa kwa kuzingatia kwamba wanakabiliwa na mitihani yao ya mwisho na hivyo kushindwa kujua hatima yao.
Shule hiyo imeelezwa kwamba inamilikiwa kwa pamoja na Wizara ya Elimu na Tamisemi.

No comments: