Monday, November 19, 2012

RAIS KIKWETE AJIFARIJI KWA IDADI NDOGO YA WALARUSHWA CCM...

Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia maelfu ya mashabiki na wanachama wa chama hicho wa mkoa wa Dar es Salaam waliomwandalia hafla ya kumpongeza jana katika Viwanja vya Mnazi Mmoja.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete ameutaka uongozi mpya wa chama hicho kujipanga kujibu mashambulizi yanayotolewa dhidi ya chama hicho, huku ikielezwa kuwa wala rushwa CCM ni asilimia 0.1 ya wanachama wake ambao asilimia 99.9 ni masikini.
Aidha, Makamu Mwenyekiti Philip Mangula na Katibu Mkuu Taifa wa chama hicho, Abdulrahaman Kinana wametangaza vita dhidi ya  wanaoendekeza rushwa ndani ya chama hicho na kubainisha kuwa  rushwa na makundi ndani ya chama hicho sasa basi.
Akizungumza katika sherehe za kuwapongeza viongozi hao wapya jijini Dar es Salaam jana, Rais Kikwete, alisema mambo mengi mabaya yamekuwa yakisemwa kila siku kuhusu chama hicho huku kukiwa hakuna hatua zozote madhubuti za kujibu tuhuma hizo.
“Namshukuru angalau Nape (Katibu Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi Nnauye) ameonesha juhudi kubwa za kuonesha kuwa CCM ipo hai na kujibu mashambulizi yanayotolewa, nawakumbusha kazi hii si ya Nape pekee ni kazi ya viongozi wote,” alisisitiza Rais Kikwete.
Alisema tuhuma mbaya dhidi ya chama hicho zimekuwa zikitolewa na vyama vya siasa vya upinzani lakini mbaya zaidi pia baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa kila kukicha vikiandika mambo mabaya kuhusu chama hicho.
“Kwa vyama vya upinzani sishangai kwa kuwa ni kazi yao kutukosoa, lakini hivi vyombo vya habari ambavyo kuanzia Januari hadi Desemba hakuna jema lolote la CCM wanaloandika kunaonesha kuna uwalakini,” alisema.
Alisema haingii akilini hata jambo jema likifanyika kama vile ujenzi wa barabara au kuimarika kwa usafiri nchini, baadhi ya vyombo vya habari  haviandiki yale mema na kazi yao ni kutafuta yale yote mabaya juu ya Serikali.
Aliitaka Sekretarieti hiyo mpya kuhakikisha kuwa kila jambo baya la CCM linapotolewa hadharani, walijibu siku hiyo, na lisilale kwa kuwa kunyamaza kimya kumeonekana kama yale yote mabaya yanayosemwa dhidi ya chama hicho ni ya kweli na sasa imani ya Watanzania juu ya chama hicho imepungua.
“Kwa sasa imani ya wananchi juu ya CCM haipo, huu ndio ukweli, lazima tujue wapi tumekosea, tujiulize nini kimeifanya CCM iwe na taswira hiyo na tujue cha kufanya, lakini kwa yale mazuri ya chama chetu tuanze kuyaanika wenyewe na mabaya tunayotupiwa jamani tusiyakumbatie, tujibu,” alisisitiza.
Alisema kuanzia sasa uongozi wa chama hicho, kazi yake kubwa itakuwa ni kurejesha imani iliyotoweka ya Watanzania juu ya chama hicho kwa kuhakikisha kinafanya mikutano ya hadhara ya mara kwa mara na kueleza maendeleo na shughuli zote za chama hicho.
“Hawa wenzetu wamekuwa wakifanya kila siku mikutano ya hadhara na wamekuwa wakitumia fursa hii ya kukutana na wananchi kutupiga madongo kweli kweli, sisi kama CCM tulikuwa hatuna mfumo huu, kuanzia sasa na sisi tunaanza kufanya mikutano na wananchi,” alisema.
Pamoja na hayo, Rais Kikwete aliwataka viongozi wapya wa chama hicho kujenga mazoea ya kukutana na makundi mbalimbali ya jamii akitolea mfano Machinga au Mamalishe ili kujua matatizo yao na kupendekeza namna ya kusaidia na si kuwaangalia wakitaabika.
Aidha alisema safari hii, wale wote waliochaguliwa kuingia Halmashauri Kuu ya chama hicho, watatumika ipasavyo kukijenga chama hicho na wataanzia na kutembelea kata, matawi, wilaya na mikoa yote kuangalia namna shughuli za chama zinavyokwenda.
“Sasa tunawatahadharisha wale wote ambao tunajua wamegombea U-NEC ili kujiongezea CV kuwa safari hii wamenoa, lazima watumike kwa kadri walivyoomba kama hawawezi watuambie kabisa,” alisisitiza.
Pia Mwenyekiti huyo, alizungumzia suala la mpasuko, makundi na rushwa ndani ya chama hicho, ambapo aliwataka wanachama wa chama hicho kuondokana na dhana ya kuchukiana na kujenga mipasuko kutokana na kuwania vyeo ambavyo si mali yao bali ya chama.
Alisema vyeo vyote vilivyopo ndani ya chama hicho kamwe si mali ya mtu bali ya chama hicho na ndio maana kuna muda wa kuviwania, hivyo kuchukiana kwa sababu ya kila mtu kutamani vyeo hivyo au kumuunga mkono mtu mwingine si haki na hakusaidii chama.
Awali akizungumza na wanachama wa chama hicho, Kinana alisema chama hicho hakijakosea kuwachagua kukiongoza na kwamba Sekretarieti hiyo imejipanga tatizo la mmomonyoko wa maadili, rushwa na tatizo la kujipangia safu ndani ya chama hicho sasa basi.
“Wapo watu hapa wamezoea kupanga washindi wao kwa sababu zao kusaidiana hapo baadaye, na wapo wanaotembeza rushwa, hawa ndio wanaoharibu chama, hatuwezi kuwa chama kinachosimamia Serikali, kinachopinga vitendo vya rushwa wakati sisi wenyewe hatuna uadilifu na tunaendekeza rushwa,” alisisitiza.
Alisema CCM ina wanachama takribani milioni tano kati yao asilimia 99.9 ni masikini lakini asilimia 0.1 kati yao ndio wala rushwa wakubwa, wapenda mizengwe na ndio wanaofanya chama hicho kizima kionekane kuwa kinapenda rushwa jambo ambalo lazima lidhibitiwe kwa kuwa si haki.
Kwa upande wake Mangula, alikiri kuwa tatizo la chama hicho hadi sasa ni rushwa hasa katika uchaguzi uliopita wa ndani ya chama hicho na kuwahakikishia wale wote waliowasilisha malalamiko yao kuhusu kutokuwepo kwa haki katika chaguzi mbalimbali kuwa yanashughulikiwa.
“Malalamiko yenu yapo kwa Katibu na tumewapa viongozi wote walioshinda lakini wanalalamikiwa miezi sita kupitia malalamiko yao na kuchunguza na ikithibitika wameshinda kwa mbinu zisizo sawa, wote ‘out’ hadi wale waliowabebea bahasha, hatutaki chama chetu kuwa cha wala rushwa, ndio tunaanza kukisafisha,” alisisitiza.
Aliwasuta wale wote waliokubali kununuliwa katika uchaguzi wa chama hicho kwamba kukubali kwao kununuliwa ni sawa na kugeuzwa sambusa au bidhaa.
“Ndio maana tunasema haya malalamiko lazima tuyafanyie kazi hatutamuonea mtu wala kumpendelea, wanachama milioni sita hatuwezi kubabaishwa na watu wachache,” alionya.

No comments: