Jamii imetahadharishwa kuwa macho na mtandao wa kuiba watoto baada ya kubainika kuwepo kwa nyumba inayotumika kuhifadhi watoto wanaoibwa jijini Dar es Salaam.Taarifa za uwepo wa nyumba hiyo na mtandao huo zimebainika baada ya kuibwa kwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Bokorani, Mtongani katika Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, Zawia Mohamed (7) (pichani), alipokuwa akitoka shuleni zaidi ya miezi minne iliyopita.
Zawia aliibwa na mtu asiyejulikana Juni 18 mwaka huu, nje ya lango la shule hiyo alipokuwa akitoka kwenda nyumbani. Hata hivyo kwa juhudi za wazazi na Polisi, alipatikana Oktoba 20 mwaka huu mkoani Singida.
Wakisimulia tukio hilo kwa nyakati tofauti hivi karibuni walipozungumza baada ya mtoto huyo kupatikana, wazazi wa mtoto huyo wanaoishi Mtoni Kwa Azizi Ally, jijini Dar es Salaam walisema uchunguzi wa Polisi na maelezo ya mtoto, umebaini kuwepo kwa mtandao hatari wa wizi wa watoto.
Kwa mujibu wa Mallya, Zawia aliibwa akitoka shuleni baada ya kuitwa na mtu asiyejulikana aliyejitambulisha kuwa ni baba mdogo na alimvusha barabara akimweleza anampeleka kumnunulia sare za shule kama zawadi yake kwa kufaulu vizuri.
Alisema mjukuu wake huyo, ambaye ni mtundu na mdadisi, alidai mtu aliyemwiba alimwambia amwite Ngasa na alikuwa akiwapa ugali kwa dagaa kila siku walipokuwa katika nyumba hiyo huku wakizuiwa kutoka nje ya nyumba hiyo.
Zawia alithibitisha hayo na kuongeza kuwa, katika nyumba hiyo aliona watu wengi wakija asubuhi katika nyumba hiyo wakipewa vibakuli ambavyo hakujuwa wanawekewa nini na aliwaona wakinywa kila mtu na kibakuli chake.
“Sisi hatukupewa, tuliona wao ndio wanakunywa, siku moja waligombana wenyewe na Ngasa alinichukua tukapakia lori tukaenda hukooo, nikakaa kwa akina God (wasamaria wema) na sikumuona tena Ngasa ndio babu na mama wakaja,” alieleza Zawia.
Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Singida, Ayub Tenge akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Linus Sunzumwa, alithibitisha tukio hilo na kutoa angalizo kwa wazazi, walimu na jamii kuwalinda watoto dhidi ya hatari ya kuibwa.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela akizungumzia kuwapo kwa mtandao huo wa wizi wa watoto, alisema ni ngumu kuthibitisha uwepo wa mtandao lakini aliahidi kulifanyia kazi suala hilo ili kubaini ukweli wake.
Akifafanua kuhusu tukio hilo, Mallya alisema msamaria mwema Sylvia (mama God) aliyemhifadhi Zawia mkoani Singida, aliwaeleza kuwa mtu huyo alifika nyumbani kwake na kudai yeye ni yatima na mke wake (mama Zawia) amekufa hivyo anatafuta Wasukuma wenzake wamhifadhi kwa muda.
Kwa mujibu wa Sylvia, mtu huyo aliyekuwa na lafudhi ya Kisukuma, wakati mwingine alishindwa kuzungumza lugha hiyo, jambo lililowapa wasiwasi na wakati wote alikuwa akimlinda Zawia ili kutompa nafasi ya kujieleza.
Baba mzazi wa Zawia, Mohamed Kassim na mama yake, Mwanahamisi, walisema taarifa za kupatikana kwa mtoto wao walizipata Oktoba 31, baada ya mtu mmoja kuwatafuta kutoka Singida.
Wazazi hao waliishukuru Polisi na vyombo vya habari kwa kuandika kuhusu tukio hilo tangu mtoto wao apotee.
No comments:
Post a Comment