Thursday, November 15, 2012

KIZIMBANI KWA KUTUPA ZAIDI YA MILIONI 15 ZA OFISI KWENYE PIPA LA TAKA...

KUSHOTO: Elaine Murray. KULIA: Innes MacDonald akionesha meseji aliyotumiwa na Elaine.
Mfanyakazi wa Posta ambaye aliiba Pauni za Uingereza 6,000 (zaidi ya Shilingi milioni 15) kwa kuibua madai pesa hizo zimepotea sababu alizitupa kwa bahati mbaya kwenye pipa la taka.
Elaine Murray mwenye miaka 44, alitumia bosi wake meseji kwenye simu akisema bila kufahamu alibeba vitu vingi sambamba na mamia ya vishina kabla ya kuzitupa fedha hizo taslimu.
Murray, mkazi wa Inverness, mwanzoni alishitakiwa kwa ubadhirifu wa Pauni za Uingereza 21,000 za Ofisi ya Posta lakini jana alipatikana na hatia katika mashitaka ya wizi wa Pauni za Uingereza 6,000 katika mahakama ya uliwali ya Inverness.
Hatahivyo, hatia yake imemchukiza Innes MacDonald, postamasta msaidizi katika Ofisi ya Posta ya Kinmylies, mjini Inverness, ambaye alisema alimwacha na upungufu wa takribani Pauni za Uingereza 22,000 tangu wakati Murray alipokuwa akifanya kazi pale.
Innes bado anajaribu kulipa deni hilo kwa kiasi cha Pauni za Uingereza 350 kila mwezi.
Innes alisema hafahamu kilichotokea katika upotevu wa kiasi hicho cha pesa.
Alisema 'tumbo lilivurugika' pale aliposoma meseji hiyo kutoka kwa Murray Septemba, 2009.
Meseji hiyo ilisomeka hivi: "Innes ninamaanisha kukwambia hivi, lakini nashindwa jinsi ya kukueleza, sababu nimepata hasara wakati nasafisha siku moja, nilikuwa na pipa kubwa la taka kutoka nyuma na kila kitu kilikuwa kimetapakaa sakafuni na nilitupia kwenye pipa pamoja na  mamia ya vishina nilivyokuwa navyo sakafuni, sijui jinsi ya kukueleza, ningeweza kukwambia pale nilipogundua."
Innes alisema: "Nilimuuliza alimaanisha nini na ilikuwa pesa kiasi gani alizotupa kwenye pipa la taka.
"Hapo ningeweza kulia. Alisema ilikuwa kama wiki 12 au zaidi zilizopita tangu alipofanya hivyo.
Innes alisema 'angeweza kulia' wakati Murray alipomtumia meseji kusema ametupa maelfu ya pauni kwenye pipa la taka.
"Tulipiga simu kwenye kampuni zote za uzoaji taka na kuendelea, lakini hazikuweza kupatikana."
Murray aliajiriwa kama meneja katika ofisi ya posta wakati huo wa wizi kati ya Januari na Septemba, 2009.
Anatarajiwa kuhukumiwa mwezi ujao.
Lakini Innes alisema atataka maelezo kutoka kwa mwendesha mashitaka kuhusu kwanini mashitaka madogo yaliletwa.
Alisema ameshalipa zaidi ya Pauni za Uingereza 16,000 tangu kugundulika upotevu huo wa pesa zaidi ya miaka mitatu iliyopita.
Innes alisema: "Ninatakiwa kuilipa Ofisi ya Posta karibu Pauni za Uingereza 22,0000 na bado ninaendelea kurejesha kiasi cha Pauni za Uingereza 350 kila mwezi. Hakika nimeghadhibika mno.
"Sababu hawa watoto wangu watatu wamenyimwa kwenda mapumzikoni kwa miaka mitatu iliyopita.
"Bado ninagharamia kwa ajili ya hili. Tayari nimerejesha Pauni za Uingereza 16,000 na natakiwa kuendelea kulipia kwa zaidi ya mwaka.
Innes alisema kama postamasta msaidizi alikuwa akiwajibika kwa fedha hizo. Alilipia mwanzoni Pauni za Uingereza 5,000 pale pesa hizo zilipobainika kupotea mara ya kwanza na anaendelea kulipia kiasi kilichobakia.
"Swali ni kwamba nini kilichotokea kuhusu pesa hizo?"

No comments: