Tuesday, November 13, 2012

KIPANYA CHAJIBAMIZA KWENYE LORI NA KUUA WATU SITA MBEYA...

Watu sita wamekufa na wengine kumi kujeruhiwa baada ya gari ya abiria waliyokuwa wanasafiria kutoka Mbeya kwenda Chimala wilayani ya Mbarali kugongana na lori la mizigo.
Ajali hiyo iliyotokea katika eneo la Mlima Nyoka nje kidogo ya Jiji la Mbeya barabara kuu ya Tanzania - Zambia majira ya saa nne asubuhi, ilihusisha gari aina ya Toyota Hiace yenye namba za usajili T 245 AMH na lori lenye T 276 AHQ.
Muuguzi wa zamu katika Hospitali ya Rufaa ambaye hakutaka jina lake liandikwe, aliwataja watu waliokufa kuwa ni  Steven Kimario (54) Mkazi wa Uyole, Sharifa Abdalah, Simon Mwakalukwa (66), Mariam Mwanginde, pamoja na  Andrew Simbeye (47),  Mkazi wa Mswisi wilayani Mbarali, wakati mwili wa mtu mmoja haujatambuliwa.
Alisema kati ya majeruhi kumi waliofikishwa hospitalini hapo, sita walitibiwa na kuruhusiwa, ambapo majeruhi wanne wanaendelea na matibabu ambao ni Elia Malowe (18), Charles Guman (53),  Dotto Tagala (44) na Fizara Kasim (28), na kwamba waliotibiwa na kuruhusiwa ni  matibabu ni Hajat Abdalah (8), Erika Januari (26), Betta Sanga (52), Maria Anania (32), Isaka Leonard (17) na Erasto Mulwale(34).
Baadhi ya watu walioshuhudia ajali hiyo, walisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa lori hilo lililokuwa likitoka Dar es Salaam kuelekea Kongo ambaye alikuwa akiyumba njia nzima.
Dereva wa lori hilo aliyejulikana kwa jina la Jofrey Msoma alikamatwa na askari wa usalama barabarani waliofika eneo la tukio.

No comments: