Tuesday, November 13, 2012

KAMPUNI ZA SIMU SASA KUBANWA KATIKA KODI...

Profesa Makame Mnyaa Mbarawa.
Serikali sasa itaanza kubana kampuni za simu za mkononi nchini katika kodi, baada ya kununua kifaa maalumu cha kujua kila senti inayotokana na simu inayoingia kwa mteja iwe ya ndani au nje ya nchi.
Kwa hatua hiyo, Serikali inatarajia kuongeza mapato katika eneo hilo la kodi hasa baada ya kuwapo na tuhuma kwamba kampuni za simu zinakwepa kodi.
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, alisema hayo jana wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya chama hicho katika Mkutano wa Nane wa CCM mjini hapa.
“Kuhusu kodi isiyo sahihi katika simu za mkononi, tutaweka kifaa maalumu cha kudhibiti hali hiii, na katika kila kampuni ya simu, kila pesa tutaijua kutokana na kifaa hicho,” alisema Profesa Mbarawa.
Nje ya ukumbi wa mkutano, Waziri huyo alisema kuwa kifaa hicho kwa lugha ya kigeni kinajulikana kwa jina la Teleco-traffic Management System, na tayari mchakato wake umeanza.
Alisema zabuni ilikwishatangazwa na kampuni 24 zikajitokeza, zikachujwa na kubaki 10 na kisha zikachujwa tena na kubaki sita, kabla ya kupata kampuni moja ambayo wanazungumza nayo sasa.
Alisema kwa kufunga kifaa hicho, kutakuwa na manufaa makuu matatu; kuangalia simu zinazopigwa kutoka nje ya nchi ili kudhibiti wajanja wanaopiga kutoka nje na simu kuonekana ni za ndani.
Profesa Mbarawa alitaja manufaa mengine kuwa ni kujua simu za ndani zinazopigwa na kudhibiti ubora wa simu.
“Mfumo kama huu umefanikiwa katika nchi za Ghana na Rwanda, na niwatoe hofu wananchi kwamba huu mfumo hauji kwa nia ya kuingilia mawasiliano ya mtu. Ni suala la kudhibiti mtandao,” alisema.
Alisema kabla ya kuanza kwa mfumo huo, kutawekwa kanuni zitakazofuatwa na watumiaji na kampuni husika.
Awali, akizungumza na wajumbe wa mkutano huo, Profesa Mbarawa alisema gharama za simu za mikononi zimezidi kupungua kutokana na kufungwa kwa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Lakini alikiri kuwa vijiji 3,000 nchini havina mawasiliano hayo, na kwamba vitapatiwa hivi karibuni, lakini nia ni ifikapo mwaka 2014, Tanzania iwe na mawasiliano ya simu za mkononi.
Pia alisema Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Mbeya (MIST) kuanzia Septemba mwaka huu, imepanda hadhi na kuwa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia.
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli alisema miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara inayoendelea nchini yenye thamani ya Sh trilioni 7.
Alisema miradi hiyo ina urefu wa kilometa 11,154, na asilimia 60 hadi 65 ya fedha za miradi hiyo ni za Serikali ya Tanzania na nchi itakuwa miongoni mwa tano za Afrika zinazotumia fedha zake kujenga barabara.
Alimsifu Rais Jakaya Kikwete kwa kufanya kazi kubwa ya kujenga barabara hizo kwa fedha za ndani na kutaka asikatishwe tamaa na watu ambao wanadai hajafanya lolote katika utawala wake.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alielezea kuhusu mafanikio makubwa ya elimu tangu kuanzia mwaka 2005, ikiwamo kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi wa shule za msingi hadi vyuo vikuu na ujenzi wa shule.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi alisema yamekuwapo mafanikio katika kudhibiti Ukimwi na malaria na pia kuongezeka kwa vyuo na watumishi wa sekta ya afya nchini.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba alisema Serikali itajenga uwanja wa ndege katika mji wa Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara ili kutumika kuvutia utalii katika ukanda wa Magharibi.
Aidha, alibainisha kuwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe, Mbeya utazinduliwa Desemba   na kwa mujibu wa Rais Kikwete, tayari umeonesha uko katika kiwango cha juu baada ya hivi karibuni kutumika kutua ndege za Jeshi.
Pia Dk Tizeba alizungumzia upanuzi wa viwanja mbalimbali vya ndege nchini, ujenzi wa bandari   na reli kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2010 – 2015.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alizungumzia mafanikio katika sekta hiyo pamoja na kuanza kwa miradi ya gesi nchini.
Awali, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali iddi na Waziri Mkuu Mizengo Pinda waliwasilisha mafanikio ya Serikali mbili za Muungano kuhusu utekelezaji wa Ilani iliyowapa ushindi mwaka 2010.
Kutokana na taarifa hiyo, wajumbe waligawanywa makundi kwa mikoa yao jana jioni na kwenda kuzijadili kabla ya leo kutolewa maazimio.

No comments: