SERIKALI YABADILI MIHULA YA MITIHANI YA SEKONDARI...

Naibu Waziri wa Elimu, Phillipo Mulugo.
Serikali imeamua kubadilisha mfumo wa mihula ya ufanyaji mitihani kwa shule za sekondari nchini, ambapo kuanzia mwakani wanafunzi wa kidato cha nne watafanya mitihani yao ya Taifa Novemba na wa kidato cha sita Mei.
Pia Serikali imesema pamoja na mwaka huu kujipanga kudhibiti udanganyifu katika mitihani kwa watakaobainika kushitakiwa na kufutiwa mitihani yao, kwa wamiliki wa shule, shule zitazuiwa kudahili wanafunzi wa kidato cha kwanza, kwa mwaka mmoja.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo alisema awali kidato cha nne walikuwa wakifanya mitihani yao Oktoba wakati kidato cha sita wakifanya Februari.
"Tayari waraka wa kubadili mihula hii ya mitihani umepitishwa ingawa kwa wanafunzi wote wa kidato cha nne na kidato cha sita wa mwaka huu haitawahusu na watafanya mitihani yao Februari kwa kidato cha sita na Oktoba kidato cha nne," alisema Mulugo.
Alisema mabadiliko hayo yametokana na mwingiliano wa kazi hasa kwa upande wa usahihishaji ambapo walimu wamekuwa wakienda kusahihisha katika miezi ambayo wanafunzi wengine bado wako shuleni, hivyo kukosa haki ya kufundishwa.
Alisema wakati wanafunzi wa kidato cha nne wakifanya mtihani wao Oktoba, Novemba walimu hulazimika kwenda kusahihisha na katika kipindi hicho, wanafunzi wa vidato vya kwanza, pili na tatu bado huwa wako shuleni hivyo kukosa kufundishwa kama kawaida.
Hali kadhalika alisema wanafunzi wa kidato cha sita wakifanya mtihani wao Februari, Machi walimu huenda kusahihisha wakati huo wanafunzi wa kidato cha tano wakiwa shuleni na hivyo nao kushindwa kufundishwa kama kawaida.
"Kubadilisha mihula hii ya mitihani kutasaidia, kwani kwa sasa wanafunzi wa kidato cha nne wakifanya mtihani Novemba, mitihani yao itasahihishwa Desemba wakati wenzao wakiwa likizo, na kwa kidato cha sita, wakifanya mtihani Mei, itasahihishwa Juni wenzao wakiwa likizo," alifafanua.
Kuhusu udanganyifu wa mitihani, Mulugo alisema Serikali inafahamu kuwa baadhi ya watahiniwa na wasimamizi wasio waaminifu, wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya udanganyifu katika mitihani.
Alisema safari hii watahiniwa watakaobainika kufanya udanganyifu watafutiwa mitihani na kufikishwa kwenye mikono ya sheria, ambapo walimu na wasimamizi nao licha ya kusimamishwa kazi zao pia watafikishwa kwenye mikono ya sheria.
"Nawakumbusha watahiniwa, kuwa kila mtu afanye mtihani kwa kujitegemea bila udanganyifu, watakaobainika watachukuliwa hatua za kinidhamu," alisema Mulugo huku akikumbusha kuwa wanafunzi 3,303 waliofutiwa mitihani mwaka jana wa kidato cha nne watarudia mitihani hiyo Novemba mwakani.
Alisema walimu na wasimamizi waliohusika na udanganifu huo, tayari wamepewa adhabu za onyo, karipio kali na kuvuliwa madaraka kwa wakuu wa shule ambapo wamiliki wa shule zilizothibitika kufanya udanganyifu, shule zao zimezuiwa kudahili wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mwaka mmoja.
Katika mtihani wa kidato cha nne utakaoanza keshokutwa, jumla ya wanafunzi 481,414 wakiwamo wavulana 263,2020 sawa na asilimia 54.67 na wasichana 218,212 sawa na asilimia 45.33 wanatarajiwa kufanya mtihani huo.

No comments: