Tuesday, October 9, 2012

MSICHANA ALAZIMIKA KUONDOLEWA TUMBO ILI KUOKOA MAISHA YAKE...

KUSHOTO: Baa iliyouza kinywaji kilichosababisha madhara. JUU: Gaby Scanlon. CHINI: Kinywaji chenye mchanganyiko wa kimiminika cha naitrojeni.
Msichana mmoja amelazimika kuondolewa tumbo kuokoa maisha yake baada ya kunywa mchanganyiko wa kinywaji chenye kimiminika cha naitrojeni.
Gaby Scanlon alikuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa akitimiza miaka 18 katika baa mjini Lancaster ndipo alipoagiza kinywaji hicho na kuanza kuhisi kushindwa kupumua.
Aliendelea kupata maumivu makali ya tumbo na kukimbizwa hospitali ambako aligundulika kuwa na matundu tumboni.
Madaktari walimfanyia upasuaji wa dharura kuondoa tumbo na kuokoa maisha yake.
Gaby, anayeishi Heysham huko Lancashire, yuko katika hali mbaya lakini anaendelea vizuri, polisi walisema.
Marafiki zake wamesema kupitia mtandao wa Twitter kwamba aliwatumia ujumbe wa maandishi wakati akitoka kwenye chumba cha upasuaji katika hospitali ya Royal Lancaster Infirmary.
Baa hiyo ambayo ilimuuzia kinywaji hicho imetajwa na Kituo cha Televisheni cha ITV News kama Oscar's iliyoko mjini Lancaster.
Ilitoa taarifa inayosema 'masikitiko makubwa' kwa kijana na kwamba 'salamu za faraja zimwendee yeye na familia yake'.
Mwezi uliopita baa hiyo ilituma picha kwenye ukurasa wake wa Facebook ya mchanganyiko wa kinywaji ambacho kimehusisha kimiminika cha naitrojeni kinachoitwa kama Pornstar Martini. Kilikuwa kinauzwa kwa Pauni za Uingereza 8.95 na toti ya shampeni, ambacho baa hiyo imekiita 'cha kustaajabisha'.
Polisi walisema baa hiyo imesitisha uuzaji wa vimiminika vyote vya mchanganyiko wa naitrojeni baada ya tukio hilo la Alhamisi.
Msemaji wa Polisi aliongeza: "Majengo yaliyohusika yalishirikiana kikamilifu na taasisis zote na wamesitisha vinywaji vinavohusisha kimiminika cha naitrojeni. Uchunguzi bado uko katika hatua zake za awali na tunaendelea kuwahoji mashuhuda kujua ukweli kamili."
Kimiminika cha naitrojeni, ambacho kuyeyuka katika nyuzijoto 196C, kimekuwa kikiongezeka umaarufu kama njia ya haraka ya kugandisha chakula na vinywaji au kuzalisha mvuke unaovutia - mbinu zilizoenezwa na mpishi wa kwenye runinga, Heston Blumenthal.
Kama kikimezwa, kimiminika hicho kinaweza kugandisha sehemu za mdomo, koo au tumbo, na kusababisha muunguzo mkubwa wa baridi ambao huharibu mkusanyiko wa seli mwilini.
Kimiminika hicho pia kinaweza kuchemsha ndani ya tumbo, na kufanya kiwango kikubwa cha mvuke ambao unaweza kusababisha uharibifu kama vitobo.

No comments: