Mbunge Mary Mwanjelwa ambaye alinusurika kwenye ajali za magari (pichani kushoto). |
Katika ajali ya Mbeya, lori la mafuta lilishindwa breki na kugonga magari matatu katika mteremko wa Mlima Iwambi – Mbalizi nje kidogo ya Jiji la Mbeya. Katika ajali hiyo iliyotokea jana saa nane mchana, Mbunge huyo, Mary Mwanjelwa alinusurika kufa baada ya gari lake, kugongwa na kuteketea kwa moto na kusababisha kifo cha Amina.
Kwa sasa Mwanjelwa amelazwa katika Hospitali Teule ya Ifisi katika wilaya ya Mbeya ambako maiti wawili walipelekwa huku wengine wanane wakihifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya.
Akizungumza kutoka eneo la ajali, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, alisema katika ajali hiyo watu zaidi ya 10 walikufa na wengine kadhaa kujeruhiwa na kwamba uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha ajali.
Baadhi ya watu walioshuhudia ajali hiyo, walidai kuwa lori hilo la mafuta lilishindwa breki na kuteremka mlima huo kwa kasi na kugonga magari matatu ikiwamo Toyota Hiace namba T 587 AHT.
Muuguzi wa Hospitali ya Ifisi, Sikitu Mbilinyi alisema Mwanjelwa analalamika zaidi maumivu mgongoni na miguu na dereva wake naye analalamikia miguu na amepasuka kichwani.
Katika hali isiyo ya kawaida, mtu mmoja alinusurika kuuawa kwa kipigo kutoka kwa wananchi wenye hasira baada ya kujaribu kuwaibia majeruhi na waliopoteza maisha katika ajali hiyo.
Wananchi waliokuwa eneo la ajali, walilalamikia tabia ya baadhi ya wamiliki wa magari kukataa kutoa msaada kwa majeruhi.
"Baadhi ya watu waliokufa walikuwa na uwezo wa kupona kama wangepatiwa msaada mapema, lakini wenye magari walikuwa wanakataa kutoa msaada," alisema mtu aliyejitambulisha kwa jina moja la John.
No comments:
Post a Comment