POLISI AJITAMBULISHA KUWA NI MTANGANYIKA...

Suala la Muungano limeibuka karibu katika kila mkutano wa Tume ya Kukusanya Maoni ya Mabadiliko ya Katiba, ambapo juzi askari Polisi Josephat Mwamunyange, alijitambulisha mbele ya mabosi wake, kuwa yeye ni Mtanganyika.
Akitoa maoni mbele ya wajumbe hao kw enye kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, ya 411 KJ, Ruhuwiko, wilayani hapa, Mwamunyange alisema yeye si Mtanzania bali Mtanganyika.
"Mimi ni Mtanganyika, si Mtanzania … Muungano unanufaisha wakubwa na kutuacha sisi masikini. Zanzibar wanatubagua, niliwahi kwenda katika safari ya mafunzo nikiwa kidato cha tatu, hata namba ya mpirani sikupewa, kwa kuwa natoka Bara," alisema Mwamunyange.
Polisi huyo wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), alitaka Muungano uvunjwe na kuongeza kuwa wakati waBara wanabaguliwa wakiwa Zanzibar, Tanzania Bara, Wazanzibari wamegeuza kuwa ‘shamba la bibi’ bila kufafanua, lakini akaongeza kuwa kwa bibi ndiko hata ukirudi nyumbani saa saba usiku, hasemi neno.
Mkazi wa kata ya Mjimwema, Clement Mtara (63) mwenye elimu ya darasa la nane, alipendekeza Muungano uendelee lakini uwe wa serikali tatu; rasilimali za Tanganyika, zitumike Tanganyika na za Zanzibar, zitumike Zanzibar.
Mkulima Alexander Mwantiku (60), ambaye elimu yake ni kidato cha nne, alipendekeza serikali tatu, lakini akafafanua kuwa Serikali ya Muungano iwe ndogo na ipewe mambo machache ya Muungano.
Erick Mkwera (40), fundi mwashi mwenye elimu ya darasa la saba, alikwenda mbali zaidi akisema kwa kuwa Zanzibar inawapa Wazanzibari vitambulisho vya ukazi, na Bara Wazanzibari watambuliwe wapewe hati za kuishi.
Mzee Mustafa Omari (87) wa kata ya Seed Farm ambaye elimu yake ni ya darasa la nne, alisema tatizo la Muungano limetokana na Watanzania Bara kuzubaa.
Akifafanua hoja yake, Mzee Omari alisema baada ya kukubaliwa kwa serikali mbili, Unguja (Zanzibar), walichagua wabunge wao, aliowaita wa Muungano kuja katika Bunge la Tanzania Bara.
Katika ufafanuzi huo, aliendelea kusema kuwa tatizo ni Watanzania Bara, ambao hawakuchagua wawakilishi wao kwenda Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
"Matokeo yake, Waunguja mambo ya Muungano wanayazungumza katika Bunge la Bara na Bara haijachagua wabunge wa kuzungumzia mambo ya Muungano katika Baraza la Wawakilishi," alisema.
Alipendekeza mfumo wa serikali mbili uendelee, lakini Watanzania Bara wachague wawakilishi watakaowasemea katika Baraza la Wawakilishi.
Hata hivyo mkazi wa kata ya Lizaboni, Peter Chakanga (43), ambaye elimu yake ni darasa la saba, alipendekeza Watanzania waliozaliwa mwaka 1964, baada ya Muungano, wautambue Muungano na atakayesema uvunjwe, aadhibiwe.
Alen Ngole (39) mwenye elimu ya darasa la saba mkazi wa kata ya Matarawe, alisema Zanzibar mtu kutoka Bara anazuiwa kununua ardhi Zanzibar mpaka aishi muda mrefu wakati Wazanzibari wakija Bara wananunua watakavyo.
Alipendekeza Wabara wafikapo Zanzibar waruhusiwe nao kununua ardhi kama wenzao wanapofika upande wa pili.
Wananchi wengi walipendekeza Muungano wa Serikali tatu, lakini waliowapinga walipendekeza Muungano wa serikali moja kwa madai kuwa serikali tatu ina gharama zaidi za uendeshaji, wakati gharama za kuendesha serikali mbili tu, zinawashinda Watanzania na wanashindwa kutoa huduma za jamii bure.

1 comment:

Anonymous said...

At thіs moment I am ready tо ԁo my breaκfast, after hаving my
breakfast сoming yet agaіn to reaԁ more nеωs.
Here is my web site 3000 loan