KIKWETE AWATAKIA SAFARI NJEMA WANAOTISHIA KUHAMA CCM...

Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete.
Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete, amesema katika kuhakikisha CCM inazidi kuwa na uhai
na kupata ushindi katika uchaguzi mkuu mwaka 2015, Kamati Kuu ya Chama hicho imeamua kuwaengua wagombea wakongwe na kutoa nafasi kwa vijana.
Pamoja na hayo, habari za ndani za vikao vya chama hicho vinavyoendelea mjini hapa, zimebainisha kuwa Mwenyekiti huyo katika kuhakikisha mizizi ya ufisadi inakatwa ndani ya chama hicho, baadhi ya vigogo wakiwamo wabunge wagombea, majina yao yamekatwa huku wengine wenye majina makubwa wakipendekezwa kuendelea.
Akifungua kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho, mjini hapa jana jioni, Rais
Kikwete alisema katika uchaguzi wa mwaka huu, chama hicho kimebahatika kupata wagombea wengi wasomi na wengi wao wakiwa vijana jambo ambalo linatia matumaini.
"Jana (juzi) CC tulimaliza saa 6.30 usiku, kazi tuliyofanya ni kubwa na tumefurahi kwamba safari hii pamoja na kupata wagombea wengi wakiwamo wasomi, wengi ni vijana, kwenye Kamati hii tumeamua kuwapa nafasi zaidi vijana na wenzetu wakongwe wakapumzike," alisema Rais Kikwete.
Alisema kati ya vijana wasomi waliojitokeza kuwania nafasi ndani ya chama hicho, wamo walio vyuoni jambo linalotia moyo kuwa bado CCM iko hai ambapo alibainisha wazi kuwa chama chochote cha siasa kikikosa mwamko wa vijana lazima kitakuwa na matatizo.
"Napenda nieleweke kuwa hatuwezi kuwa na chama cha watu wazima pekee, chama chenye mfumo huo hakitakuwa na mfumo mzuri wa uongozi, tumefanya hivi ikiwa ni fursa ya kukipa chama chetu uhai na taswira mpya lakini kubwa zaidi ushindi wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2014 na Uchaguzi Mkuu 2015," alisisitiza.
Alisema katika uchaguzi huo wa ndani wa chama, wanachokitarajia ni kupata timu ya viongozi wenye uadilifu, shupavu, hodari na wenye kukitetea chama, kwa maana nyingine alisisitiza kuwapo timu ya ushindi wa chama na si ushindi wa mtu.
"Na nasisitiza, hatutaki kiongozi mwenye ndimi mbili, maana nasikia kuna watu wanatishia eti wakikatwa huku kwenye ugombea wanakwenda vyama vingine, nasema hivi, wenye nia hiyo waende kwa sababu hadi kufikia kutishia hivyo ina maana tayari wana nafasi huko, tunawatakia kila la heri," alisisitiza.
Aliwataka wagombea watakaoshindwa kwenye uchaguzi huo kutokata tamaa, kwa kuwa kushindwa kwao leo hakumaanishi hawawezi, bali ni kutokana na nafasi finyu lakini pia umuhimu wa mabadiliko na kutumia usemi kuwa kuvunjika kwa koleo si mwisho wa uhunzi. "Hata Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere (Julius) alisema chama kwanza utu baadaye."
Aidha, Mwenyekiti huyo alizungumzia suala la baadhi ya wagombea wa chama hicho kudaiwa kutoa rushwa hali ambayo inageuza uchaguzi huo kama biashara na kuwa wagombea wa namna hiyo hawafai kwa kuwa hawajiamini, wala kuthamini chama, bali uongozi na kuwahakikishia kuwa safari hii Takukuru haitakuwa mbali nao na wakikamatwa wasimlaumu.
"Sheria ya rushwa inaanzia kwenye chama, najua wapo watu ambao wanakifanya chama chetu kisemwe sana, nawaomba sana tutumie fursa hii kubadilika na kukipa chama chetu heshima," alisema.
Kikwete alionya wagombea ambao wamesababisha uchaguzi wa CCM kugeuka vurugu za silaha na kuwatanabaishia kuwa wamekifedhehesha chama hicho. "Watu mnafikia hatua ya kutumia mishale, bastola na mikuki, kugombea NEC tu mnashikiana silaha kweli? Jamani uchaguzi si vita."
Wakati NEC ikianza, Katibu Mkuu wa chama hicho, Wilson Mukama alisema idadi halisi ya
wajumbe wa NEC ni 216 na waliohudhuria ni 196.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya kikao cha Kamati Kuu (CC), majina yaliyoondolewa yakiwamo ya wabunge lengo ni kukata mizizi ya ufisadi iliyoota ndani ya chama hicho tawala.
Hata hivyo chanzo cha habari kilisema kwamba hayo ni mapendekezo ya Kamati hiyo na huenda mabadiliko yakatokea.
Chanzo hicho cha habari kilichoomba kutoandikwa jina kilisema kazi kubwa ambayo imefanywa na Kamati ya Usalama na Maadili ya Chama hicho iliungwa mkono na CC huku wajumbe wa vikao hivyo viwili wakimpongeza Rais Kikwete kwa kufanya uamuzi mgumu.
Inadaiwa Kamati ilikata majina yote ya wabunge waliowania nafasi hiyo, ambao walihusika katika utiaji saini Azimio la kumn’goa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda lililoanzishwa hivi karibuni bungeni na Mbunge wa Kigoma Kaskazini Kabwe Zitto, endapo hakutafanyika marekebisho ya Baraza la Mawaziri.
Wabunge hao walisaini fomu maalumu iliyolenga Pinda kuwaondoa mawaziri ambao wizara zao zilitajwa katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Kamati za Bunge ambapo ilikuwa ikihitajika sahihi za wabunge 70.
Wabunge hao ni Nimrod Mkono ambaye ni Mbunge wa Musoma Vijijini ambaye anawania nafasi ya uenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa; Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe ambaye anagombea ujumbe wa Nec kupitia Wilaya ya Ludewa.
Kwa mujibu wa wabunge hao walikuwa wakishinikiza kuondolewa kwa mawaziri hao ni Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu, Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Mkuchika, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu na Waziri wa Viwanda na Biashara, Cyril Chami.
Habari hizo zilidai kuwa walioenguliwa na Kamati Kuu ambao pia Kamati ya Maadili ilipendekeza waenguliwe, yumo Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina aliyekuwa akiwania uenyekiti wa Mkoa wa Simiyu, Mbunge wa Kahama, James Lembeli na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja ambao wote walikuwa wakiwania uenyekiti wa Mkoa wa Shinyanga.
Wengine walioenguliwa na CC ni Mbunge wa Nzega, Dk Khamis Kigwangallah na kada maarufu wa CCM, Hussein Bashe, ambao wote walikuwa wakiwania ujumbe wa NEC kupitia Wilaya ya Nzega.
Pia Mbunge wa Viti Maalum, Sara Msafiri ambaye alikuwa akiwania ujumbe wa NEC na Mbunge wa Viti Maalumu, Munde Tambwe ambaye alikuwa akiwania uenyekiti wa Umoja wa Wanawake, Mkoa wa Tabora.
Habari hizo zilisema sababu ya kuondolewa kwa wabunge Munde na Sara ni kutokana na kashfa ya rushwa kwa wabunge inayoendelea kuchunguzwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Kilimanjaro, Vick Swai  ambaye alikuwa akitetea nafasi yake.
Katika Jumuiya ya Vijana (UVCCM), walioenguliwa ni pamoja na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dodoma, Anthony Mavunde, Mbunge wa Ilala Musa Azzan ‘Zungu’ aliyekuwa akiwania uenyekiti Wazazi.
"Wengi walioondolewa kwa kuwa wengi wao ni mizizi ya ufisadi, na kwa kuwa ukishaondoa mizizi unabaki mti lazima mti ukauke, tuliona hakuna haja ya kuleta kishindo kikubwa kwa kuondoa waliotajwa sana kwa ufisadi, ila matokeo mtayaona baadaye," kilisema chanzo hicho.
Chanzo chetu cha habari ndani ya vikao hivyo kilidai kuwa aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa anayewania nafasi ya ujumbe wa NEC kupitia Wilaya ya Monduli na Mbunge wa Bariadi Mashariki anayegombea pia ujumbe wa NEC kupitia Bariadi, Andrew Chenge imependekeza waendelee kugombea nafasi hizo.
Wengine ni Mbunge wa Same Mashariki Anne Kilango-Malecela, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba na Mayrose Majinge wote wanawania uenyekiti UWT Taifa
wamependekezwa kuendelea.
NEC imeendelea na vikao vyake hadi jana usiku ambapo leo majina zaidi ya waliomwagwa na waliopita yanatarajiwa kutolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM, Nape Nnauye.

No comments: