MCHUNGAJI MTIKILA ASHINDA KESI YA KUMDHALILISHA RAIS KIKWETE...


Mchungaji Christopher Mtikila.
Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu jana imemwachia huru Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila aliyekuwa akishitakiwa kuchapisha na kusambaza waraka wa uchochezi dhidi ya Serikali na Rais Jakaya Kikwete. 
Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Ilvin Mugeta alisema ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashitaka mahakamani hapo, haukutosha kumuona Mtikila kuwa na hatia ya kutenda kosa hilo.
Akisoma maelezo ya kesi hiyo yaliyopo katika hukumu, Mgeta alidai kuwa Mchungaji Mtikila kati ya Novemba 1 mwaka 2009 na Aprili 17 mwaka 2010, jijini Dar es Salaam kwa nia ya uchochezi alisambaza kwa umma nyaraka zilizosomeka: “Kikwete kuuangamiza Ukristo, Wakristo waungane kumuweka mtu Ikulu”.
Hakimu alisema pamoja na kwamba maneno hayo yanaonesha uchochezi, upande wa mashitaka uliokuwa ukiwakilishwa na Jamhuri katika kesi hiyo, umeshindwa kuthibitisha namna gani kauli hiyo imekuwa ya uchochezi kwa kuwa machapisho hayo hayajaleta madhara yoyote katika jamii.
Huku akitolea mfano baadhi ya vifungu vilivyowahi kutumika katika hukumu mbalimbali ikiwemo ya kesi moja ya nchini Uganda, Mgeta alisema kimsingi malalamiko yaliyokuwa yametolewa dhidi ya Mtikila, hayakuweza kutetewa na ushahidi wa upande wa mashitaka uliokuwa ukiwasilishwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali Tumaini Kweka.
Katika utetezi wake dhidi ya kesi hiyo Mtikila alipanga kuwaita mashahidi 10 na baadaye kuishia kumuita shahidi mmoja aliyekuwa Mpigapicha Mkuu wa magazeti ya Mwananchi Communications, Mpoki Bukuku aliyepeleka kielelezo cha ushahidi ambacho ni gazeti la Mwananchi la Agosti 9 mwaka 2009, lenye kichwa cha habari “Mtikila apiga kampeni kanisani kumpinga JK... achunguzwa na polisi kumwaga sumu Rais asichaguliwe 2010”. 
Bukuku alidai kuwa habari hiyo ilikuwa ikiripoti kilichotokea mkoani Mwanza katika mkutano wa maaskofu, lengo likiwa ni kuelimisha jamii na kwamba anajiamini  kuwa habari haikuwa na tatizo lolote kwa sababu  polisi hawajalalamika.
Baada ya hakimu kutoa hukumu ya kesi hiyo na kutoka nje ya chumba cha Mahakama Mtikila alisimama na kupaza sauti ‘Haleluya’ kwa zaidi ya mara tatu huku baadhi ya watu alioongozana nao wakiitikia Amen.
Hata hivyo furaha ya Mchungaji huyo iliingia doa baada ya mtu mwingine, Gotum Ndunguru, kujitokeza mahakamani hapo akitaka akamatwe kwa ajili ya kesi ya madai. Alikuwa na RB no KMR/RB/10482/2012 aliyoifungua katika Kituo cha Polisi Mbezi Mwisho dhidi ya Mtikila.
Ilizuka tafrani kwa dakika kadhaa iliyovuta watu waliokuwepo baada ya Mtikila kumgeuzia kibao Ndunguru akidai kuwa alikimbia dhamana katika kesi aliyoifungua dhidi yake, na hivyo kuzua mabishano kati ya askari, Ndunguru na Mtikila.
“Naomba huyu mtu akamatwe, ni mvamizi mkubwa wa maeneo ya watu, ameshanipora viwanja vyangu vitatu, kavunja nyumba yangu ya thamani kubwa na sasa ametishia kuniua, Polisi mkamateni ili aende kituoni sasa hivi,” alisikika akisema Ndunguru.
Mtikila aliwaambia askari, “Nyinyi hamuwezi kunikamata mtu kama mimi, mnanijua mimi ni nani, mimi nafika Polisi kwa kupigiwa simu na IGP Said Mwema au askari mwingine mwenye cheo cha SSP,” alisema Mtikila huku akiondoka katika viwanja vya Mahakama hiyo.

2 comments:

Anonymous said...

Wow, that's what I was looking for, what a material! present here at this blog, thanks admin of this web site.
My webpage : 2000 loan

Anonymous said...

If sοmе onе ωiѕhеs eхpеrt νiеω on
the topic οf bloggіng and site-builԁing then і аdvіsе hіm/hеr tо pay a visit thiѕ wеbsite, Кeeρ up the goοd ϳob.
Also visit my web page :: bad credit loans