Sunday, August 12, 2012

WAZIRI KAGASHEKI AHOJI UADILIFU WA MCHUNGAJI MSIGWA...

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchingaji Peter Msigwa.
Siku moja baada ya kufikishwa kwenye Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na Maadili kwa kudaiwa kutoa maneno ya uongo bungeni, Mbunge wa Iringa Mjini na Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA), ameendelea kubwana zaidi kwa tukio hilo.
Hata baada ya Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai kuagiza Mchungaji Msigwa kupelekwa kwenye kamati hiyo, bado jana Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki alitumia muda mwingi kumshambulia Mchungaji Msigwa akimtuhumu kusema maneno mengi ya uongo kupitia hotuba yake.
Kupitia nafasi hiyo, Balozi Kagasheki alihoji uadilifu wa Mchungaji huyo, kutokana na tabia ya kutochunguza mambo na kujikuta akiwa mpotoshaji.
Akijibu hoja mbalimbali za wabunge waliochangia mjadala wa wizara yake iliyojadiliwa kwa siku mbili, Kagasheki alianza na hoja za kambi ya upinzani iliyokuwa imeichambua Serikali kwa kudai imejaa uzembe na pia inahusika na matukio ya ujangili nchini kutokana na kuwakingia kifua watuhumiwa.
Balozi Kagasheki, akijibu hoja hizo alisema taarifa ya Mchungaji Msigwa bungeni juzi ilijaa uongo mwingi, ikitoa mfano waziri huyo kutajwa akifurahia kupigwa picha wakati akipokea faru watatu kutoka Uingereza.
Alisema: "Kuna mengine yanasemwa haya ukweli. Nikianza na mimi mwenyewe, natajwa kuwa nilionekana nikipokea faru Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, jambo ambalo si la kweli. Sikuwepo kabisa, huu ni uzushi.
Faru, sikuwepo. Huu ni upotoshaji, sijui kwa nini watu hawafanyi utafiti. Aidha, niweke wazi kwamba, Serikali haijaelemewa na wala si lelemana. Ila nikiri kwamba mitandao ya ujangili ni mikubwa, ila serikali haijalala, inafanya kazi."
Aliendelea kusema kuwa, ameshangazwa na uongo wa waziwazi kutoka kwa Mchungaji, ambaye alistahili kuwa mfano wa kuigwa na jamii kwa kuwa mkweli.
"Hii hotuba imetolewa na mtu ambaye nilitegemea angekuwa mkweli, hapa tunamzungumzia Mchungaji. Waheshimiwa wabunge, mchungaji kwa nafasi yake, kwa shughuli zake ndani ya jamii, ni mtu wa kusema ukweli, mtu wa kukemea uongo na matendo yasiyofaa, lakini sasa kama mchungaji mwenyewe anakuwa anaeneza habari ambazo hazina usahihi…basi hii ni hatari kubwa."
"Lakini niseme, kwa kuwa mchungaji huyu kapotosha, haina maana kwamba wachungaji wote ni wapotoshaji, siyo sahihi.
"Aidha, hotuba aliyoitoa inaonekana dhahiri imejaa chuki dhidi ya serikali ya CCM… , lakini hapa si mahala pake, ni mahala pa kuweka mambo sawa hivyo tunapaswa kushirikiana kwa faida ya Watanzania," alisema.
Lakini baadaye, mchungaji Msigwa aliomba mwongozo wa Mwenyekiti wa Kikao cha jana, Mussa Zungu, akitaka mwongozo kwa kuitwa mwongo na pia kitendo hicho kukihusisha na uchungaji wake ambalo alisema hakupewa bungeni, hivyo si sahihi kuhusisha uchungaji wake na mambo ya bungeni.
Zungu aliahidi kumpa majibu ya mwongozo katika vikao vijavyo vya bunge.
Tukio hilo limekuja baada ya juzi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi kuibua uongo wa mchungaji huyo, baada ya kuliambia bunge kuwa, Mwenyekiti wa CCM wilayani Karatu ni jangili, lakini analindwa na Serikali ya CCM.Alimtaja kuwa anaitwa Mzee Lazaro.
Lakini Lukuvi aliibuka na kusema kuwa, Lazaro anayetajwa kuhusika na kashfa hizo huku akitajwa kuwa ni Mwenyekiti wa CCM wilaya Karatu, si Mwenyekiti wa CCM kama ambavyo Mchungaji Msigwa aliliambia bunge alipokuwa anawasilisha hotuba yake mapema juzi.
Lakini baada ya ya mapumziko ya mchana, Lukuvi alisimama na kuliambia bunge; "Nataka kulithibitishia Bunge na kama wote tunamtanguliza mbele Mungu…kuwa, Mwenyekiti wa CCM Karatu haitwi Mzee Lazaro kama ilivyoandikwa na kusomwa bungeni na Mchungaji Msigwa. "Mwenyekiti wa CCM Karatu anaitwa John Zakaria Tipa...huyu ndiye Mwenyekiti wa CCM tunayemjua sisi kwa wilaya ya Karatu.
"Wengi wanamjua, Sendeka anamjua, na hata mbunge wa Karatu (Israel Natse wa Chadema) anamjua…huyo aliyemtaja kama Mwenyekiti wa CCM ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Karatu kwa tiketi ya Chadema, lakini labda niwasaidie…kama wanahusisha na jambo hili la ujangiri, Mwenyekiti wetu ni msafi, hana bunduki wala kashfa hizo."
Baada ya uthibitisho wake, alimtaka Naibu Spika kutoka mwongozo huku akionya tabia ya uzushi bungeni.

No comments: