Sunday, August 12, 2012

SERIKALI YAAHIDI KUGEUZA MSITU WA MABWE PANDE KUWA 'PEPONI'...

Sehemu ya eneo la msitu wa Mabwe Pande ambayo imegawiwa viwanja kwa ajili ya makazi ya watu waliohamishwa kutoka mabondeni, Dar es Salaam.
Serikali inakusudia kuupandisha hadhi Msitu wa Pande, Dar es Salaam ili uianze kutumika kwa shughuli za utalii badala ya kuachwa utumiwe vibaya na wahalifu wanaoutumia msitu huo kutesa watu na hata kuua.
Hatua hiyo itasaidia kukomesha vitendo vya uhalifu yakiwemo mauaji na mateso kwa watu yanayotokea mara kwa mara ndani ya msitu huo.
Hayo yalisemwa bungeni jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) aliyetaka kujua kama kuna mpango wa kubadili matumizi ya pori hilo ambalo limekuwa la mateso na ukatili.
Mnyika ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo, akiuliza, alisema: "Pori la Msitu wa Pande limekuwa tayari kwa usalama, hapa ndipo yalipotokea mauaji ya ile kesi ya Zombe (Abdallah), ndiko walikotekwa akina Dk Ulimboka (Stephen) na hivi karibuni kuna mtu ameuawa.
"Je, kuna mpango wowote wa kubadili matumizi ili eneo hilo litumike kwa ajili ya utalii wa ndani?"
Akijibu, Kagasheki alisema: "Hatuwezi kuliacha kabisa liendelee kuwa pori na unyanyasaji na mateso kwa mtu yeyote. Ni nia ya wizara kwa kushirikiana na TTB (Bodi ya Utalii Tanzania) na wadau wengine wakiwemo wabunge wa Dar es Salaam ili kuhakikisha tunalipandisha hadhi hili pori ili liweze kusaidia utalii wa Dar es Salaam.
"Kama vile ambavyo tungependa kuona wananchi wa Dar es Salaam, lakini pili tunaazimia kuongeza utalii wa Dar es Salaam kwa upande wa usafiri wa boti na mambo ya kale," alisema.

No comments: