Tuesday, August 14, 2012

WALIOHUSIKA KUTOROSHA TWIGA WIZARA YA MALIASILI WATIMULIWA...

Serikali, baada ya kufanya uchunguzi wa kina imetangaza kuwafukuza kazi vigogo wa Wizara ya Maliasili na Utalii, waliohusika na kashfa ya ukamataji na usafirishaji wa wanyamapori hai nje ya nchi.
Miongoni mwao yumo Obeid Mbangwa, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori aliyekuwa amesimamishwa tangu Novemba 17 mwaka jana, kupisha uchunguzi wa usafirishaji wa wanyamapori hai 136 wenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 100 na ndege 16 uliofanyika Novemba 24, mwaka 2010.
Wanyama hao walisafirishwa kwenda nje ya nchi kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Uamuzi huo ulitangazwa bungeni jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki ambaye alisema licha ya Mbangwa na wenzake kufukuzwa kazi, sasa watakabiliwa na hatua za kisheria.
Alisema kabla ya kufikia uamuzi huo, tume huru mbili zilifanya uchunguzi wa kina na kujiridhisha kuwa wahusika walikiuka sheria katika utekelezaji wa majukumu yao, hivyo kusisitiza kwamba hakuna aliyeonewa.
Mbangwa alikuwa Mkurugenzi wa Idara hiyo akiteuliwa hivi karibuni kuchukua nafasi ya mtangulizi wake Erasmus Tarimo, aliyestaafu kwa mujibu wa sheria. Wakati Tarimo akiwa Mkurugenzi, Mbangwa alikuwa Mkurugenzi Msaidizi (Matumizi Endelevu).
Kagasheki aliwataja wengine waliofukuzwa kuwa ni Simon Gwera na Frank Msemi ambao ni maofisa uwindaji wa kitalii na utalii wa picha katika kituo cha Arusha.
Aidha, Serikali imemshusha cheo Bonaventura Midala, Mkurugenzi Msaidizi, Uendelezaji Wanyamapori ambaye wakati wanyama hao wakisafirishwa, alikuwa Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Kuzuia Ujangili.
Waziri Kagasheki alisema Midala amehukumiwa kutokana na kutochukua hatua kikamilifu ambazo zingeweza kuzuia utoroshwaji wanyama hao.
Alisisitiza, kuwa chini ya utawala wake zitafanyika juhudi za kila aina kulinda rasilimali za nchi ili zimfae kila Mtanzania, badala ya hali inayoonekana sasa ya kunufaisha wajanja wachache.
Wakati hao wakifukuzwa na kushushwa vyeo, Kagasheki alisema wizara yake imewapa onyo kali la maandishi maofisa wanyamapori wawili, Martha Msemo na Anthonia Anthony waliokuwa wanashughulikia leseni katika ofisi ya uwindaji wa kitalii na Utalii wa Picha, Msemo akiwa kituo cha Arusha na Anthony akiwa Dar es Salaam.
Adhabu kama hiyo imetolewa pia kwa Mkuu wa Kituo cha Uwindaji wa Kitalii na Utalii wa Picha Arusha, Sylvanus Okudo, kwa kushindwa kufuatilia na kupata maelekezo ya Mkurugenzi wa Wanyamapori kuhusu mtumishi wake aliyekiuka utoaji vibali na pia kushindwa kupeleka taarifa kwa Katibu Mkuu ili mhusika achukuliwe hatua za kinidhamu.
Maofisa ambao bado uchunguzi wao unaendelea ni Mohammed Madehele wa Ofisi ya Matumizi Endelevu ya Wanyamapori na Mariam Nyallu wa Kituo cha Uwindaji wa Kitalii na Utalii wa Picha, Arusha.
Kutokana na kashfa hiyo ya usafirishaji wanyama hai nje ya nchi, Serikali mwishoni mwa mwaka jana ilipiga marufuku biashara ya kukamata na kusafirisha wanyamapori kwenda nje ya nchi.
Hatua hiyo ilitangazwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda bungeni baada ya wabunge kulaani uhalifu uliofanywa na wajanja ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii huku wakitaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya watu waliohusika, kwa kuwa limeidhalilisha Serikali na vyombo vyake vya Dola vyenye majukumu ya kusimamia usalama wa nchi.
Habari za kutoroshwa wanyama zilianza kusikika tangu mwanzoni mwa mwaka jana, lakini mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii uliibua maswali mazito dhidi ya Serikali ambayo hatimaye ilitoa majibu na kuchukua hatua.
Moja ya hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kusitisha usafirishaji wanyama hai na pia kusimamishwa baadhi ya maofisa wa wizara husika.
Tanzania inategemea utalii kwa asilimia takribani 17 ya mapato yake na wanyama ni sehemu muhimu ya vivutio vyake.

No comments: