Thursday, August 23, 2012

VERONICA MPANGALA AIBUKA KIDEDEA SHINDANO LA BIBI BOMBA...


Bibi Veronica Mpangala ndiye mshindi wa Shindano la kumsaka Bibi Bomba linaloendeshwa na Kituo cha Clouds Tv kwa mwaka 2012 na kuwabwaga wenzake saba waliokuwa wakiwania taji hilo.
Kwa ushindi huo ambao ulitokana na kura zilizopigwa na mashabiki mbalimbali, Veronica amejinyakulia zawadi ya kitita cha Shilingi milioni 5/- taslimu kutoka kwa wadhamini wa Shindano hilo, Benki ya NMB.
Sherehe ya kutangaza washindi wa shindano hilo ambayo iliendeshwa na mshereheshaji Babu wa Kitaa na kurushwa moja kwa moja na kituo hicho cha televisheni, ilifanyika kwenye makao makuu ya Kampuni ya Clouds Media Group, Mikocheni, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watu kadhaa maarufu akiwamo mwigizaji filamu maarufu, Jacob Steven 'JB', mchekeshaji Steve Nyerere pamoja na watangazaji kadhaa wa Clouds Media.
Washindi wengine walioshika nafasi tatu za juu ni pamoja na Anna Said aliyejinyakulia kitita cha Shilingi milioni 3/- taslimu kwa kushika nafasi ya pili na Shilingi milioni 1.5/- zilikwenda kwa Nasra Mohammed kutoka Zanzibar aliyeshika nafasi ya tatu.
Wadhamini wengine wa Shindano hilo ambao wameahidi kuendelea na udhamini wao mwakani ni pamoja na Kampuni ya Simu za Mikononi ya Zantel na familia ya Janguo iliyotoa gari aina ya Limoussine kwa ajili ya kuwatembeza mabibi hao.

No comments: