Saturday, August 11, 2012

PEDESHEE PAPA MSOFE ASHITAKIWA KWA MAUAJI...


Mfanyabiashara wa Dar es Salaam Marijani Msofe (50) maarufu kama Papaa Msofe amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashitaka ya mauaji.
Msofe alifikishwa mahakamani hapo jana saa 3:30 asubuhi akiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Agness Mchome.
Alisomewa mashitaka yake saa 5:30 asubuhi na Wakili Mwandamizi wa Serikali Tumaini Kweka.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, Novemba 6, mwaka jana katika eneo la Magomeni Mapipa Wilaya ya Kinondoni, Msofe alimuua Onesphory Kitoli, na ameshitakiwa chini ya Kifungu cha 196 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 .
Hakimu Mchome alisema, mshitakiwa hatatakiwa kujibu mashitaka kwa kuwa Mahakama hiyo haistahili kusikiliza kesi ya mauaji isipokuwa Mahakama Kuu.
Mshitakiwa alirudishwa rumande na kuondoka mahakamani hapo saa 6:05 mchana akiwa kwenye gari lenye namba za usajili T 1447 akisindikizwa na askari wanne.
Ndugu wa mshitakiwa waliokuwa mahakamani hapo walishindwa kujizuia na kumwaga machozi wakati Papaa Msofe alipokuwa akirudishwa rumande. Kesi itatajwa tena Agosti 23 mwaka huu.
Kesi hiyo imefunguliwa katika Mahakama hiyo kwa hatua ya upelelezi na baadaye itahamishiwa katika Mahakama Kuu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.

No comments: