Wednesday, August 15, 2012

NYOKA ALIYEVUNJA REKODI ANASWA AKIWA NA UREFU WA FUTI 17, MAYAI 87...

Nyoka wa aina ya Burmese mwenye urefu wa futi 17 na inchi 7 aliyevunja rekodi kwa kubeba mayai 87 amekamatwa mjini Florida.
Akiwa na uzito unaofikia ratili 164.5, ni nyoka mkubwa wa aina yake kupatikana nchini humo na ni uthibitisho wa jinsi viumbe kutoka nje wanavyotishia wanyamapori wa ndani, wamesema watafiti.
"Hiki kitu cha ajabu mno, ana upana wa takribani futi," alisema Kenneth Krysko kutoka Makumbusho ya Florida ya Historia Asili. "Inamaanisha nyoka hawa wanaishi kwa muda mrefu msituni, hakuna cha wakuwazuia na kwamba viumbehai asilia wako hatarini."
Nyoka mkubwa wa aina hiyo alikamatwa kwa mara ya kwanza na watafiti kwenye Hifadhi ya Taifa ya Everglades mwezi Machi. Baada ya kuchukuliwa vipimo na kufungwa vichunguza nyendo alirejeshwa hifadhini katika kile watafiti walichokiita 'Nyoka wa Yuda."
Watafiti walifuatilia nyendo za nyoka huyo kujifunza kuhusu jinsi viumbe hao walivyovamia eneo hilo.
Nyoka aina ya Burmese, asili yake kusini mwa Asia, waliwasili Marekani miaka 30 iliyopita kama sehemu ya viwanda vya kutengenezea sumu ya wanyama. Japo nyoka hao hawana sumu, wana nguvu mno kuweza kuua binadamu kwa kuwabana pumzi.
Rekodi zilizopita za nyoka huyo aina ya Burmese aliyekamatwa msituni ilikuwa futi 16.8 na mayai 85, kwa mujibu wa watafiti.

No comments: