Friday, August 10, 2012

MAONI YA KATIBA YAHUJUMIWA...

M
wenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amevishutumu vyama vya siasa, asasi za kiraia pamoja na wanaharakati, kwa kuwashawishi na kuwapa mambo ya kuzungumza baadhi ya wananchi wanaoenda kutoa maoni mbele ya tume hiyo.
Jaji Warioba alisema makundi hayo kwa kisingizio cha kutoa elimu ya uraia juu ya Katiba, yamekuwa yanawapa miongozo ya kuzungumza baadhi ya wananchi, hali inayowafanya wananchi hao washindwe kutetea hoja hizo wanapoombwa kutoa ufafanuzi wa mambo waliyozungumza.
Hata hivyo, Jaji Warioba alisema katika awamu ya kwanza ya ukusanyaji wa maoni uliofanywa katika mikoa minane, Tume hiyo tayari imeanza kupata dalili na picha ya aina ya Katiba wanayoitaka wananchi kutokana na maoni waliyokusanya kutoka kwa baadhi yao waliotoa maoni yao bila kushawishiwa na vikundi, vyama au taasisi.
Alisema licha ya kuwa wananchi wengi hawaifahamu Katiba, lakini wanapotoa maoni yao wamekuwa wakizungumzia mambo yanayowahusu ambayo alisema ndio msingi wa kuandikwa kwa Katiba mpya.
Alisema baadhi ya maoni ya wananchi pia yanaangukia katika mambo 13 yaliyoainishwa na tume hiyo ambayo wananchi wamechangia.
Akizungumza kuhusu suala la vyama vya siasa na wanaharakati kutoa elimu, Jaji Warioba alisema asasi hizo zinapoenda kutoa elimu, zinawaambia wananchi cha kuzungumza na waligundua hivyo kwa vile suala moja linalozungumzwa katika mkoa mmoja hilo hilo linazungumzwa katika mkoa mwingine.
"Haiwezekani suala hilo lizungumzwe Shinyanga na Kagera walizungumze hilo hilo, hii inaonesha wamepewa miongozo ya kuzungumza. Lakini safari hii sisi tunasema watu waseme yaliyo moyoni mwao, hayo ya itikadi na uanaharakati watapata nafasi baadaye.
"Vyama vya siasa, taasisi na asasi mbalimbali waache Watanzania watoe maoni yao kwa uhuru bila kulazimishwa. Wananchi wanapaswa kutambua kwamba Katiba inayoandikwa ndiyo nguzo na mwelekeo wa maisha yao ya kila siku, wasikubali kutumiwa kwa namna yoyote ile na kikundi chochote katika kuwasilisha maoni yao kwa tume," alisema Jaji Warioba.
Katika awamu ya kwanza mikoa iliyohusika ni Pwani, Dodoma, Manyara, Kagera, Shinyanga, Tanga, Kusini Unguja na Kusini Pemba. Mikutano iliyofanyika ni 386.
Tume pia ilifanya mikutano maalumu na taasisi za dini na vyombo vya ulinzi na usalama. Awamu ya pili itaanza Agosti 26, mwaka huu katika ya Mbeya, Morogoro, Lindi, Ruvuma, Kigoma, Katavi na Mwanza.
Mwenyekiti huyo alisema vyama vya siasa na wanaharakati wasidhani kuwa kwenda kutoa elimu ni kwenda kumfundisha mwananchi cha kuzungumza; badala yake wawape elimu itakayowawezesha wananchi kufahamu kile wanachokitaka kiwamo kwenye Katiba.
Alisema mwananchi aliyeelekezwa cha kusema anapoombwa ufafanuzi, hawezi kuzungumza zaidi; lakini pale anaposema yaliyo moyoni mwake, hata ofisa wa tume akitaka ufafanuzi wananchi wamekuwa wanafafanua vizuri.
Alisema maeneo ambayo wananchi wametoa maoni zaidi ni kwenye ardhi, kilimo, elimu, huduma za jamii, pensheni kwa wazee na wasiojiweza, mfumo wa uongozi wanaoutaka, madaraka ya Rais, Bunge, aina ya wabunge wanaowataka, Mahakama na misingi ya kitaifa.
Lakini pia alisema wananchi wametoa maoni kuhusu Muungano ambao wamo wanaotaka uvunjike, wengine wanataka Serikali mbili, wengine moja, wengine tatu na wengine wanataka Muungano wa mkataba wenye Serikali mbili.
Kuhusu changamoto zinazoikabili tume hiyo, Jaji Warioba alisema awali wananchi wengi walikuwa hawajitokezi kwenye mikutano wakati mikutano inapoanza, lakini kadiri muda unavyoenda wananchi walikuwa wengi.
Hata hivyo, alikiri kuwa wanawake hawajitokezi kwa wingi kutoa maoni ingawa wanahudhuria mikutano ya tume.
Alitoa takwimu kuwa wastani wa wananchi 188,679 walihudhuria mikutano ya tume katika mikoa hiyo minane. Wananchi 17,440 walitoa maoni yao kwa njia ya kuzungumza kwenye mikutano, wengine 29,180 walitoa maoni yao kwa njia ya maandishi.
Changamoto nyingine ni shughuli za Tume kuingiliana na shughuli nyingine za kijamii kama vile ibada na magulio. Pia changamoto nyingine ni baadhi ya wananchi kutegemea njia moja tu ya kuwasilisha maoni kwa kuzungumza wakati kuna njia nyingine kama barua pepe na posta.
Kuhusu muda, Jaji Warioba alisema miezi 18 kweli ni michache, lakini changamoto hiyo tume imeikubali na watajihidi kufanya kazi kuhakikisha wanakamilisha kazi hiyo kwa muda waliopangiwa.
Alisema wakitathmini hali ya siasa ilivyo nchini kwa sasa, tume hiyo itajitahidi kufanya kazi ili uchaguzi ujao wa mwaka 2015 ufanywe huku tayari kukiwa na katiba mpya. "Tunataka utulivu katika nchi yetu, hivyo uchaguzi wa 2015 tunataka ufanyike tukiwa na Katiba mpya, kutokana na hali ya siasa iliyopo," alisema.

No comments: