Tuesday, August 14, 2012

MAALIM SEIF ACHOCHEA ZANZIBAR KUDAI KITI UMOJA WA MATAIFA...

Siasa za aina ya Muungano; uwe wa serikali mbili au tatu sasa zimechukua sura mpya, kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Seif Sharif Hamad kusisitiza umuhimu wa Zanzibar kurudishiwa kiti chake katika Umoja wa Mataifa (UN) kama ilivyokuwa kabla ya Muungano.
Ili kufanikisha hilo, Hamad ametaka Wazanzibari kujitokeza kwa wingi katika awamu ya pili ya kutoa maoni ya Katiba, huku akisisitiza Zanzibar kuwa na kiti hicho UN kama ilivyokuwa baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964.
Akizungumza jana na wananchi na wafuasi wa CUF Pemba, Hamad alisema Tanzania itapata Katiba mpya Aprili mwaka 2014 ambapo kwa upande wa Zanzibar mchakato huo unahusu wananchi moja kwa moja katika suala la Muungano na marekebisho yake.
Alisema wakati umefika kwa Wazanzibari kukirudisha kiti hicho kilichokuwapo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, 1964.
"Mchakato wa marekebisho ya Katiba kwa upande wa Zanzibar unahusu moja kwa moja Muungano...wakati umefika Wazanzibari warudishe kiti chao UN," alisema Hamad.
Hata hivyo, ili nchi iwe na kiti UN, ni lazima iwe Dola huru au Dola kamili na hivyo haiwezi kujitambulisha kuwa ndani ya Dola nyingine, kwa maana kwamba Zanzibar haiwezi kuwa Dola huru na kuwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kuvunja Muungano. Kwa ukweli huo, Zanzibar haiwezi kuwa na kiti UN bila kuvunja Muungano.
Hamad alitaka wananchi na viongozi wa vyama vya siasa kuachana na misimamo wa vyama vya siasa na kuweka mbele alichoita ni maslahi ya Taifa katika suala la kuona Zanzibar inakuwa Dola kamili inayojitegemea.
"Katiba ya nchi ni mali ya wananchi na si chama cha siasa, lakini najua kila chama kina Katiba yake, lakini katika suala la marekebisho ya Katiba ni bora wananchi wakaweka maslahi ya Taifa mbele," alisema Hamad.
Msimamo wa CUF, haujaeleza wazi kuwa Muungano uvunjwe bali umeweka wazi kuwa ubadilishwe uwe wa serikali tatu wakati msimamo wa CCM ukidumisha Muungano wa serikali mbili.
Hamad katika ‘kampeni’ hiyo, alitaka wananchi wa Pemba kujitayarisha kutoa maoni ya marekebisho ya Katiba awamu ya pili bila ya wasiwasi wala woga na hakuna mtu atakayewawajibisha katika hilo.
Mapema Hamad alitaka wananchi wajitokeze kwa wingi wakati wa Sensa ya Watu na Makazi Agosti 26 kwa lengo la kuliwezesha Taifa kupata takwimu sahihi zitakazosaidia kuleta maendeleo.
Alisema takwimu za nchi zinahitaji kukusanywa vizuri katika maeneo mbali mbali ambapo Serikali itajua mahitaji ya wananchi ikiwamo maendeleo ya sekta ya afya, elimu na uchumi kwa jumla.
"Wananchi jitokezeni kwa wingi katika Sensa ya Watu na Makazi kwa ajili ya kuiwezesha Serikali kutoa huduma zake muhimu za elimu, afya na maendeleo ya uchumi na kujikwamua na matatizo ya umasikini," alisema.

No comments: