Tuesday, August 14, 2012

HELIKOPTA ZA UGANDA ZILIZOPOTEA ZAPATIKANA...


Helikopta mbili za Uganda kati ya nne zilizopotea zimekutwa zimeungua katika msitu wa mlima Kenya.
Mabaki ya helikopta hizo za kijeshi zilikutwa jana asubuhi na maofisa Wanyapori wa Kenya.
Mkurugenzi wa Kitengo hicho cha Wanyapori, Julius Kipngetich alisema “tumezikuta helikopta zimeungua na tunafanya mpango wa helikopta nyingine ziweze kufika kwenye eneo la tukio kwa uokoaji na kuendelea kuzitafuta nyingine”.
Hata hivyo timu ya polisi, wanajeshi na maofisa wanyapori wanaendelea kutafuta helikopta nyingine mbili na watu waliokuwepo ndani katika maeneo ya Ukasi in Mwingi, Masinga, Laikipia na Kora.
Watu saba waliokuwepo kwenye helikopta hizo wameokolewa na kupelekwa kwenye ngome ya jeshi ya Nanyuki huku uokoaji ukisitishwa kwa muda kutokana na hali ya hewa kuwa mbaya. Kila helikopta ilikuwa na wanajeshi watano.
Msemaji wa Jeshi la Wananchi la Uganda, Kanali Felix Kulayigye alisema katika helikopta iliyoelekea Mogadishu, Somalia ilikuwa na wanajeshi 13.
“Tunataka kuwashukuru wenzetu Wakenya kwa operesheni yao ya kuokoa wanajeshi wetu ”, alisema.
Helikopta hizo zilikuwa zikielekea Somalia kwa ajili ya kuongeza nguvu kwa majeshi ya Umoja wa Afrika yaliyopo nchini humo kupambana na Al Shabaab na kulinda amani.
Kanali  Kulayigye alikanusha taarifa kuwa tukio hilo limetokea kutokana na mafunzo ya chini ya kiwango wanaopewa wanajeshi.
Helikopta hizo tatu aina ya Mi-24 hazitaweza kutengenezeka na kutumika tena. Ni sehemu ya helikopta sita zilizonunuliwa na Serikali chini ya amri ya Rais Yoweri Museveni ya mwaka 2011 ambapo kulitumika Sh za Uganda bilioni 960 kutoka Benki Kuu bila idhini ya Bunge.

No comments: