Monday, August 20, 2012

KUTANA NA JAMAA ANAYEFANYA KAZI NGUMU ZAIDI KWA UJIRA KIDUCHU...

Kama unafikiri kazi yako ni mbaya basi wasiliana na Devi Lal.
Mpigambizi huyo kwenye mifereji ya maji machafu kutoka Delhi, India, hulipwa ujira kidogo wa Pauni za Uingereza 3.50 kwa siku kuzibua uchafu katika mifereji mjini humo.
Devi mwenye miaka 43, hupatiwa chupa ya pombe haramu kumpandisha 'mzuka' kabla ya kuanza majukumu yake hayo.
Katika namna ya ajabu, jiji hilo halijishughulishi kumpatia nguo za kujikinga hivyo Devi na wenzake wanalazimika kutumia masaa kadhaa kwa siku wakiwa ndani ya maji machafu wakiwa na nguo zao za ndani pekee.
Kwa mujibu wa Harnam Singh, Mwenyekiti wa Delhi Safai Karamchari Commision (Tume ya Wasafishaji Mji wa Delhi) takribani asilimia 70 ya wazamiaji wa kienyeji hufa katika kazi hiyo.
Inakadiriwa wazamiaji 61 wamekufa katika kipindi cha miezi sita pekee.
Licha ya India kuzuia zoezi hilo mwaka 1993, Wakala wa Serikali bado wanatumia maelfu ya wasafishaji wa kienyeji kuzibua mifereji nchini humo.
India ni miongoni mwa nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi duniani. Lakini umaskini bado unasambaa kwa kasi inayokadiriwa kufikia asilimia 42.5 ya watoto wenye maradhi ya utapiamlo.
Kwa mujibu wa taarifa za mwaka 2010 kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa, inakadiriwa asilimia 37.2 ya Wahindi wanaishi chini ya mstari wa umaskini katika nchini hiyo huku asilimia 68.7 wakiwa wanaishi kwa kipato cha chini ya Dola za Marekani 2 kwa siku.
Mapema wiki hii, Waziri Mkuu wa India Manmohan Singh alitangaza nchi yake itatumia Pauni za Uingereza milioni 52 kwa ajili ya kupeleka chombo kwenye sayari ya Mars.

No comments: