Friday, August 17, 2012

ASKARI WA PIKIPIKI WAGONGA WATOTO WAWILI, WAFYATUA RISASI...

Polisi wamelazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi usiku kucha kijijini Mahuta, Tandahimba, mkoani hapa baada ya kuzuka vurugu za wananchi waliochoma moto pikipiki ya Jeshi hilo inayodaiwa kugonga watoto kijijini hapo. 
Habari kutoka kijijini hapo zilizothibitishwa na Mkuu wa Wilaya hiyo jana, zilisema polisi walilazimika kufyatua mabomu hayo usiku wa kuamkia jana, ili kutuliza jazba za wananchi zilizotokana na askari polisi kugonga watoto wawili na kujeruhi mwananchi kwa risasi.
Shuhuda wa tukio hilo aliliambia gazeti hili kwamba Polisi wawili wakiwa kwenye pikipiki mmoja akiwa na bunduki walikuwa wakimkimbiza mwendesha bodaboda ili kumkamata na ndipo walipogonga watoto hao waliokuwa wamepakizana kwenye baiskeli. 
"Baada ya kuanguka, polisi walisimama haraka ili kukimbia, lakini hawakufanikiwa, kwani wananchi walishawazingira…mwenye silaha baada ya kuona watu wanaongezeka alifyatua risasi na kumjeruhi pajani Bwatam Nambenge (22).
"Polisi hao walikimbilia katika kituo cha Polisi na kutelekeza pikipiki, wananchi
hao waliichoma moto, na kisha kuzingira kituo cha Polisi wakiwa na mawe kutaka kuadhibu askari waliosababisha ajali hiyo," alidai Mohamedi Chivalavala shuhuda wa tukio hilo.
Shuhuda huyo alitaja watoto waliogongwa na pikipiki ya polisi hao kuwa ni Bibie Hassan (15) na Faima Mkumba (9) wote wakazi wa Mahuta.
Kwa mujibu wa Mganga wa Kituo cha Afya Mahuta, Edina Chibwana, watoto hao wanaendela na matibabu vizuri sambamba na majeruhi wa risasi.
Habari zaidi zinadai kuwa muda mfupi baadaye, polisi kutoka Newala na Mtwara waliwasili kijijini hapo kusaidia wenzao na walifyatua mabomu ya kutoa machozi na kusababisha hofu kwa wananchi ambao baadhi yao walikimbia makazi yao.
"Hatukulala kabisa, polisi wamekesha wakifyatua mabomu ya kutoa machozi, hakuna amani kabisa, hali ni tete…watoto na vikongwe wamelala porini," alidai Chivalavala
Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Ponsiano Nyami ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya, alithibitisha kutokea tukio hilo na kuongeza kuwa atatoa taarifa baada ya kurudi eneo la tukio. 
"Kuna taarifa zenye mkanganyiko, kwa mfano wapo wanaosema polisi wamempiga risasi raia kwa makusudi, wengine wanasema alijeruhiwa kwa bahati mbaya, zipo taarifa za kituo kuchomwa moto, wengine wanasema kiko salama. 
"Wapo wanaosema watoto wako mahututi wengine wanaendelea vizuri, wapo wanaosema askari mmoja yuko hoi wengine wanasema anaendelea vizuri; sasa ni lazima nifike huko ili nitoe taarifa yenye usahihi," alisema Nyami.

No comments: