Tuesday, June 5, 2012

VIONGOZI WA KUNDI LA UAMSHO WAJISALIMISHA POLISI...


Baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Uamsho Zanzibar wakiwa katika picha ya pamoja na mwandishi wa habari wa gazeti la Jamhuri, Manyerere Jackton.
Viongozi wanne wa Jumuiya ya Mihadhara ya Dini ya Uamsho wanaotuhumiwa kwa uchochezi wa vurugu za wiki iliyopita mjini Zanzibar, jana wamejisalimisha Polisi na kuhojiwa kwa saa kadhaa kabla ya kuachiwa kwa masharti.
Viongozi waliojisalimisha ni Katibu wa jumuiya hiyo, Shehe Abdallah Saidi (45) ambaye ni mkazi wa Misufini na Ofisa Usalama wa jumuiya hiyo, Haji Sadifa (51), mkazi wa Mwembenjugu.
Wengine ni Shehe Suleiman Juma (62), mkazi wa Makadara na Shehe Fikirini Majaliwa (47), mkazi wa Jang’ombe.
Viongozi hao pamoja na wafuasi wao, walijisalimisha jana asubuhi katika Kituo cha Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar na kuhojiwa kwa muda kabla ya kupelekwa Makao Makuu ya Upelelezi Zanzibar kwa mahojiano zaidi na baadaye kuachiwa kwa dhamana.
Tangu kutokea kwa vurugu hizo zilizosababisha baadhi ya wafuasi wa jumuiya hiyo mjini Zanzibar kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zao, viongozi hao na wafuasi wao hawakupatikana.

Mara baada ya vurugu hizo za wiki iliyopita, Kamishna wa Polisi
Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alisema kuwa Polisi
itahakikisha wale wote waliochochea vurugu hizo wanakamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu mashitaka yao.
Katika vurugu hizo zilizodumu kwa siku tatu, baadhi ya makanisa yalichomwa moto na mali nyingine za madukani
kuporwa na nyingine kuharibiwa na wafuasi wa jumuiya hiyo.
Polisi Zanzibar imeendelea kutoa mwito kwa viongozi
wengine walioshiriki katika vurugu hizo kujisalimisha wenyewe Polisi badala ya kusubiri kutafutwa.
Hadi sasa watuhumiwa 78 wakiwemo viongozi wa jumuiya ya hiyo wamekamatwa na kufikishwa mahakamani ambapo baadhi yao wameachiliwa kwa dhamana na wengine wakipelekwa rumande kwa kukosa wadhamini wenye kuaminika hadi Juni 11, mwaka huu kesi yao itakapotajwa tena.
Jumuiya hiyo imekuwa ikidai kuitishwe kwa kura ya maoni kuhusu Muungano huku ikihamasisha Wazanzibari kuukataa Mungano. Mbali na kuhamasisha waukatae Muungano, jumuiya hiyo inadaiwa kuhusika katika uchomaji wa makanisa kadhaa Zanzibar.

No comments: