Rais wa zamani Hosni Mubarak ametendewa haki, kwa kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.
Mubarak alipatikana na hatia ya kuua waandamanaji wakati wa ghasia za mwaka jana za kupinga utawala wake zilizomsababisha kung’oka madarakani, hatua ambayo inathibitisha anguko la mtu ambaye alitawala nchi kama mali yake kwa miongo mitatu.
Adhabu hiyo kali dhidi ya kiongozi huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 84 ilionekana kutaka kumaliza mgawanyiko unaoonekana dhahiri katika kinyang’anyiro cha urais, ambao unaonekana kumwelemea aliyekuwa waziri wake mkuu anayepambana na mgombea wa Muslim Brotherhood.
Mubarak ambaye ni kiongozi wa kwanza wa Kiarabu kushitakiwa nchini mwake, jana alibaki kimya ndani ya kizimba cha Mahakama huku mmoja wa wanawe wa kiume walioonekana kuwa na nguvu sana enzi zake, akihuzunika na mwanawe mkubwa, Alaa akikariri mistari ya Korani kimyakimya.
Kiongozi huyo wa zamani baada ya hukumu hiyo alisafirishwa kwa helikopta kutoka katika chuo cha Polisi ambacho kilitumika kama Mahakama jijini hapa.
Vurugu kati ya wafuasi wa Mubarak na wapinzani wake zilizuka nje na ndani ya Mahakama baada ya hukumu kusomwa, zikiashiria mikingamo iliyogubika nchi tangu alipong’olewa Februari 11 mwaka jana.
Maelfu ya polisi wa kutuliza ghasia walizingira jengo hilo kuzuia waandamanaji na jamaa za waliouawa wakati wa ghasia hizo kulikaribia. Mamia ya watu walisimama nje wakipeperusha bendera za Misri na kuimba nyimbo wakidai “fidia”. Baadhi yao waliweka picha ya Mubarak kwenye chokaa na wengine kuikanyaga.
Mubarak na wanawe wa kiume wawili-Gamal na Alaa- walifutiwa mashitaka ya rushwa, lakini wanawe hao bado wanakabiliwa na kesi zingine tofauti za biashara. Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Habib el-Adly naye alihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa mauaji ya waandamanaji. Maofisa wengine sita wa usalama waliachiwa huru.
Jaji Ahmed Rifaat alitoa taarifa yenye maneno makali kabla ya kutoa hukumu hizo. Mubarak , ambaye alikuwa amevalia miwani ya giza na koti la kahawia juu ya shati na washitakiwa wenzake, walikuwa ndani ya kizimba cha chuma.
Jaji Rifaat alielezea enzi za Mubarak kama “miaka 30 ya giza” na “njozi zilizogubikwa kiza” ambazo zilimalizika pale Wamisri walipoamka na kudai mabadiliko.
“Walidai demokrasia kwa amani kutoka kwa watawala ambao waling’ang’ania madaraka kwa nguvu zao zote,” alisema Jaji.
Rifaat ambaye alikuwa akiendesha Mahakama hiyo kwa mara ya mwisho kabla ya kustaafu, alisema Mubarak na el-Adly hawakuchukua hatua yoyote kuzuia mauaji katika siku 18 za machafuko ambayo yalishuhudia vikosi vya usalama vikishambulia na kuua waandamanaji wasio na silaha.
Zaidi ya waandamanaji 850 waliuawa, wengi wao kwa risasi jijini hapa na katika miji mingine mikubwa.
Hukumu dhidi ya Mubarak imekuja siku chache baada ya uchaguzi wa rais kutarajiwa kurudiwa Juni 16 na 17 kati ya aliyepata kuwa Waziri Mkuu wa Mubarak, Ahmed Shafiq na adui mkubwa wa Mubarak, kiongozi wa Chama cha Muslim Brotherhood, Mohammed Morsi.
Anakuwa Rais wa pili wa Afrika kuhukumiwa kifungo baada ya hivi karibuni aliyekuwa Rais wa Liberia, Charles Taylor kuhukumiwa kifungo cha miaka 50 jela na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) The Hague, kwa kupatikana na hatia ya kushiriki mauaji nchini Sierra Leone.
Taylor alisaidia waasi nchini Sierra Leone kufanya mauaji huku akipewa almasi kwa kubadilishana na silaha.

No comments:
Post a Comment