Friday, May 25, 2012

SINEMA YA "TRANSFORMERS 3" YAMSABABISHIA ULEMAVU WA MILELE...



Msichana ambaye amejikuta akipata majeraha ya kudumu ya ubongo wakati wa utengenezaji filamu ya 'Transformers 3' amepokea kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 18.5 kwa ajili ya matibabu jana.
Gabriella Cedillo mwenye miaka 24, alilazimika kuchukuliwa kwa ndege kupelekwa hospitali baada ya kugongwa na chuma kizito kichwani alipokuwa akiendesha gari wakati wa utengenezaji filamu hiyo mwaka 2010.
Chuma hicho kilichomoka kutoka kwenye moja ya mashine juu na kuangukia kioo cha mbele cha gari aina ya Toyota alilokuwa akiendesha Gabriella kwenye eneo la Hammond, mjini Indiana, walikokuwa wakipiga picha za filamu hiyo.
Binti huyo alichukuliwa kwa helikopta hadi hospitali ya jirani na moja kwa moja akafanyiwa upasuaji kufuatia majeraha makubwa aliyopata kichwani.
Wanasheria wake wamesema "hali imekuwa mbaya sana kufuatia juhudi za kuepusha chuma hicho kisiangukie kwenye gari kushindikana.
Wanasheria wa Gabriella wameongeza kuwa watengenezaji filamu hiyo Paramount Pictures na DreamWork's Studios walifanya kila wamezalo kukwepa kulipa gharama za matibabu na walipeleka hati kadhaa za kisheria kupinga kumlipa fidia binti huyo, imeelezwa.
Jaji wa Mahakama ya Cook County jana ameidhinisha malipo ya fidia ya mamilioni ya Dola za Kimarekani.
Wakati wa ajali hiyo mwaka 2010, shahidi alisema: "Waya uliofungwa chuma hicho ulifyatuka na kuelekea upande wa magharibi ambako walikuwapo na kujibamiza kwenye gari la binti huyo, na kuharibu kabisa sehemu ya mbele.
"Kwa upande tuliokuwapo sikufahamu kama aligongwa na chuma kile palepale au la… gari liliendelea kwenda."
Gabriella hakuwa mwigizaji rasmi lakini alikuwa ni kati ya waigizaji wa ziada tu kwenye filamu hiyo.
Katika siku hiyo mbaya na ngumu ya upigaji picha, alikuwa mwigizaji wa ziada ambaye alichagua kuendesha gari lake mwenyewe, aina ya Toyota Sedan la mwaka 2006.
"Sisi sio watu tuliosomea," kilisema chanzo kimoja cha habari kutoka ndani ya timu hiyo ya uigizaji.
"Waliwalipa waigizaji wa ziada waliotumia magari yao pesa ya ziada Dola za Kimarekani 25 kwa siku.
"Hatukupewa tahadhari kuhusu hatari iliyokuwa mbele yao dhidi ya kiasi cha pesa tunacholipwa kwa kuwapo mahali hapo, hailipi!"
Kaka wa Gabriella alisema kwamba dada yake alikuwa akifanya kazi kama karani wa benki mpaka wakati wa tukio hilo, lakini aliamua kutumia fursa hiyo kujipenyeza kwenye tasnia ya filamu.
"Hiyo haikuwa mara yake ya kwanza kucheza filamu kama mwigizaji wa ziada," alisema kaka huyo Adam, bila kufafanua alifanya hivyo kwenye filamu zipi hasa.
"Siku zote alikuwa akitaka kucheza filamu."

No comments: