Saturday, May 26, 2012

SABABU ZA MTOTO KUMSHIKA KICHWA OBAMA ZABAINIKA...

Picha moja ya mtoto akimshika kichwa Rais Barak Obama kwenye ofisi moja imezusha maswali mengi miongoni mwa watu kwenye mitandao ya intaneti.
Imeonesha mtoto wa miaka mitano aliyevalia shati jeupe na tai yenye michirizi mekundu akigusa juu ya kichwa cha Rais, kwa umakini na kujiamini usoni mwake.
Lakini sasa, sababu za mtoto huyo kufanya hivyo zimebainika.
Picha hiyo ni ya mwaka 2009, miezi mitano baada ya Obama kuanza Urais wake na ilipigwa na mmoja wa wafanyakazi wa Ikulu, Pete Souza katika tukio la kushitukiza.
Stori hiyo ya kufurahisha kwanza ilibainishwa na gazeti la New York Times. Mtoto huyo aliyefahamika kwa jina la Jacob, alijumuika na baba yake, Bwana Carlton Philadelphia, askari wa zamani ambaye anahama kikazi Ikulu hapo na kwenda Wizara ya Mambo ya Ndani.
Gazeti hilo lilibainisha kwamba ilikuwa ni utaratibu wa kawaida kwa watumishi wanaoondoka hapo kikazi kuomba kupiga picha na Rais.
Mara picha ilipopigwa, familia ilijiandaa kuondoka, lakini mara watoto wawili wa Bwana Philadelphia walimuuliza Rais swali moja.
Kabla ya tukio hilo, mtoto wake Jacob alimuuliza baba yake kwa aibu kama nywele za baba huyo zinafanana na za Rais.
Jacob alizungumza kabla ya kaka yake, Isaac, akisema kwa sauti chini: "Nataka kujua kama nywele zangu ni sawa na zako."
Rais hakusikia, na akamtaka kijana huyo mwenye miaka mitano kurudia swali. Ndipo Rais akajibu: "Kwanini usizishike na kujionea mwenyewe."
Lilikuwa tukio ambapo Rais aliinama na kuruhusu mtoto huyo kushika kichwa chake na kupata hisia kuhusu nywele zake. Akamhamasisha Jacob kwa kusema, "Ziguse, uone!"
Hapo ndipo mpigapicha Souza akapiga picha hiyo iliyosisimua, ambayo gazeti la Times limeita, "Tukio lisilo la kawaida."
Baada ya kuachia kichwa cha Rais, Jacob alitoa suluhisho kwa wenzake waliokuwa hapo. "Ndio, zinafanana," alihitimisha.
Picha hiyo kwa sasa imekuwa kivutio ambapo imewekwa sehemu mbalimbali za maofisi ya Ikulu na pia kwenye sebule ya nyumbani kwa Bwana Philadelphia.

No comments: