JUU: David Simpson akiwa na rafiki yake. CHINI: Kiongozi wa majeshi ya waasi wa LRA, Joseph Kony ambaye anasakwa usiku na mchana. KULIA: David Simpson akiwa kazini.
Raia mmoja wa Uingereza juzi alikabiliwa na adhabu ya kifo baada ya kushitakiwa kwa makosa ya mauaji ya halaiki baada ya kuvumbuliwa miili ya watu 13 kwenye msitu mmoja barani Afrika.David Simpson mweney miaka 24, meneja wa kampuni kubwa ya uwindaji, alikamatwa wiki sita zilizopita katika Jamhuri ya Afrika ya Kati baada ya taarifa za vifo kuwafikia polisi.
Alijikuta akitupwa jela kwa tuhuma za mauaji hayo, ambayo yanaaminika kufanywa na wafuasi wa kundi la waasi linaloongozwa na Joseph Kony.
Simpson, ambaye kampuni yake inahudumia wateja matajiri nafasi za kuua simba, chui na nyati, amekuwa akishikiliwa jela pamoja na wafuasi wake 80 katika kile alichoelezea kama 'naota'.
Mzaliwa huyo wa Yorkshire, kijana wa mkulima alilieleza gazeti moja kuwa ameshitakiwa kwa makosa ya jinai ambayo adhabu yake ni kifo kwenye nchi hiyo yenye makovu ya vita.
Akizungumza juzi kwa njia ya simu kutokea gerezani, alisema: "Kwa wiki sita wamenishikilia bila kuwa na chembe ya ushahidi.
"Na sasa nimelazimishwa kusaini kipande cha karatasi kinachoeleza ninashitakiwa kwa mauaji ya watu 13.
"Ni jambo la ajabu. Kila mmoja anajua sihusiki kabisa. Wanajua ni Kony ndiye aliyefanya hivyo.
"Yote ni sababu ya pesa. Wanafikiri kwa sababu mimi ni mtu mweupe, lazima nitakuwa tajiri.
"Mara waliponikamata kwa mara ya kwanza, dhamana yangu ilikuwa Euro milioni moja, jambo ambalo ni la kushangaza sana.
"Sifahamu kitakachotokea. Ni kama naota.
"Ninalala sakafuni bila mablanketi wala mashuka. Nataka jambo hili limalizike."
Mkuu wa Majeshi ya Waasi wa Uganda, Kony, kiongozi wa kundi la Lord’s Resistance Army, anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai kwa makosa yake dhidi ya haki za binadamu ikiwamo udhalilishaji wa maelfu ya watoto ambao aliwalazimisha kuwa wanajeshi au watumwa wa ngono.
Vikosi vyake vimehusika na mauaji ya mamia ya watu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambako inaaminika ndiko alikojificha.
Ametawala sana vichwa vya habari katika vyombo vya habari vya kimataifa baada ya video yake ya matukio ya uvunjaji sheria kutazamwa zaidi ya mara milioni 90.
Simpson alikuja Afrika miaka miwili iliyopita kujifunza maisha mapya mbali na familia yake ya wakulima mjini Gillamoor, North Yorkshire.
Licha ya kuwa meneja wa kampuni moja ya uwindaji, pia alikuwa rubani wa kampuni akisafirisha wageni na kuchukua mazao yao.
Alikuwa akisaidia wenzake kutengeneza njia kwenye msitu mnene maeneo ya akiba kusini mwa eneo la uwindaji la kampuni yake Machi 23, ndipo walipokuta miili ya wafanyakazi jirani na mgodi wa dhahabu.
Miili ya wanaume hao ilikuwa imefungwa pamoja kwenye makundi manne na kuuawa kwa kumwagiwa maji ya moto. Walikatwakatwa mapanga na kupigwa kwa fimbo.
Alisema: "Ilikuwa ni kitu cha kutisha kuona. Waliuawa kwa njia ya unyama wa hali ya juu, wakifungwa pamoja kwa mafungu, sura zikitazama chini.
"Niliwataarifu polisi lakini sikufikiria mara mbili kwamba watanigeuzia kibao.
"Kony ameua na kuwabaka wanavijiji wengi hapa. Nimekuta miili ya wanawake na wanawake aliowashikilia mateka na kuwaua.
"Niliongoza msafara wa wachunguzi kwenye eneo ya mauaji na kuchukua picha kadhaa kwa kutumia simu zao za mikononi, kama sehemu ya upelelezi wao."
Polisi katika mjini mkuu, Bangui, walimshikilia Simpson na Bosi wake kutoka Sweden, Erik Mararv baada ya masaa sita ya mahojiano pale kwa hiari yao walipokwenda kutoa taarifa ya mauaji hayo ya halaiki. Mararv pia anashikiliwa na polisi.
Kampuni yake, Cawa inatoa nafasi ya watalii kuwinda wanyama katika hifadhi kwa gharama ya maelfu ya Pauni za Uingereza, ambapo gharama za kuua simba ni kati ya Pauni 20,000.
Kaka wa Simpson, Paul mwenye miaka 22, ambaye anaishi na wazazi wao, Peter mwenye miaka 57, na Vicky mwenye miaka 55 kwenye shamba lao, alisema: "Natumaini polisi watabaini ukweli na kumwachia huru."

No comments:
Post a Comment