KUSHOTO: Khadija Shah. JUU: Dawa za kulevya aina ya heroin ambazo alikutwa nazo Khadija. CHINI: Polisi wa Uwanja wa Ndege wa Islamadab ambao walimkamata Khadija.
Mwanamke mjamzito wa Uingereza anakabiliwa na adhabu ya kifo baada ya kukutwa na akijaribu kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye thamani ya Pauni za Uingereza milioni 3.2.Khadija Shah mwenye miaka 25 alikuwa akijaribu kurejea Birmingham pamoja na watoto wake wawili pale alipokamatwa na maofisa wa polisi waliogundua zaidi ya kilo 63 za dawa zilizofichwa ndani ya nguo kwenye masanduku matatu tofauti.
Alidai amemsaidia kubeba mabegi hayo wanaume aliokutana nao Pakistan na hakujua kilichokuwamo ndani yake.
Mamlaka zilizoko kwenye mji wa Islamabad wanawashuku wanaume hao walikuwa ni wahuni.
Mzigo huo unaaminika kuwa mkubwa zaidi wa Daraja A za dawa za kulevya kuwahi kukamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Islamabad ukielekea kwenye mitaa ya Uingereza.
Chini ya Sheria za Pakistan, yeyote anayekamatwa na dawa za kulevya zenye uzito unaofikia kilo 10 anakabiliwa na adhabu ya kifungo jela na adhabu ya juu kabisa ni kifo.
Alikuwa mapumzikoni nchini Pakistan kwa mwezi mmoja na nusu, akiishi na ndugu zake mjini Mirpur, kabla ya kuhamia nyumba ya wageni iliyoko mjini Islamabad.
Watoto wake, Aleesha Munir mwenye miaka minne na Ibrahim Munir mwenye miaka sita, aliwazaa kwenye mahusiano yake ya awali, na sasa amepewa ujauzito na rafiki yake wa kiume, Amar Ali.
Bw. Ali, ambaye amepanga kwenda Pakistan kuchukua watoto wake, alibainisha kuwa 'kwa upumbavu' wake alikubali kuchukua mabegi hayo licha ya kumkataza kufanya hivyo.
Alisema aliongea na Khadija kwa simu kabla hajaondoka kwenda uwanja wa ndege.
Khadija akamwambia kuna wanaume wamemfuata na kumwomba kama anaweza kuwasaidia kupeleka mabegi yao Uingereza.
Akasema: "Asubuhi hii wakati natoka katika nyumba ya wageni kuelekea uwanja wa ndege, mtu mmoja alikuja kwenye nyumba ya wageni na kunitaka nibebe mabegi na kuwapelekea jamaa zake mjini Birmingham. Sikufahamu kilichokuwa ndani."
Nyumbani kwa Khadija jana, Bw. Ali alisema: "Alitarajiwa kurudi nyumbani leo.
"Niliongea naye kwa njia ya simu lakini ikakatika. Nilimweleza asifanye hivyo. Nilimwambia asimwamini yeyote.
"Nilipokuwa kule kila mmoja anataka uwe rafiki yake sababu unatoka Uingereza. Watu wanataka wakuweke kwenye himaya yao ili uwabebee masanduku yao urudipo Uingereza.
"Nilisema, 'Hakikisha huchukui mzigo wowote wa mtu'." Akiongea na Ali huku akiwa chini ya ulinzi wa polisi, Khadija alidai kupigwa na polisi na kuhofia usalama wa watoto wake.
Maofisa wa ngazi za juu wa Islamabad walisema Khadija alionekana kuwa mwenye wasiwasi alipokuwa uwanja wa ndege.
"Mwenendo wake ulitufanya kukagua mizigo yake kwa makini," alisema mmoja wa maofisa.
"Masanduku matatu yalikuwa yamejazwa vizuri vitu vya nyumbani na nguo. Tulipokagua kwa makini, ndipo dawa hizo za kulevya zikagundulika."

No comments:
Post a Comment