Monday, May 7, 2012

MIILI YA WATU 23 YAKUTWA IMETUNDIKWA KWENYE DARAJA...

Miili ya watu 23 imekutwa ikining'inia kwenye daraja ama kutelekezwa na kutupwa katika mpaka wa mjini wa Nuevo Laredo, mahali ambako wauza dawa za kulevya wanapigana vita vikali vya kumwaga damu.
Mamlaka zimekuta miili tisa ya wahanga wakiwamo wanawake wanne wakiwa wamening'inizwa kando ya njia inayoelekea barabara kuu, alisema ofisa wa mji wa Tamaulipas aliyeongea kwa sharti la kutotajwa jina sababu si msemaji rasmi wa suala hilo.
Masaa kadhaa baadaye, polisi waliona vichwa 14 vya binadamu ndani ya majokofu nje ya ukumbi wa jiji kando yake kukiwa na ujumbe wa vitisho. Miili hiyo 14 ilikutwa kwenye mifuko myeusi ya plastiki ndani ya gari lililotelekezwa karibu na daraja la kimataifa, ofisa huyo alisema.
Ofisa huyo hakueleza kilichoandikwa katika ujumbe huo wa vitisho, au kuhamasisha mauaji.
Lakini mji huo ulio mpakani kutokea Laredo, Texas hivi karibuni ulikubwa na vita vipya kati ya Zetas, kundi linaloongozwa na wapiganaji wa vikosi maalumu vya majeshi ya Mexico, na kundi lenye nguvu la Sinaloa ambavyo vimeunganisha nguvu na kundi la Gulf ambao walijiengua kutoka Zetas.
Vyombo vya habari vya ndani vilichapisha picha za miili nane iliyotapakaa damu, baadhi ikiwa imezibwa sura imetundikwa darajani huku ikiwa na ujumbe wa vitisho kwa kundi la Gulf.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Alejandro Poire alikutana na Kiongozi wa Jimbo la Tamaulipas, Egidio Torre Cantu Ijumaa iliyopita na kuafikiana kupeleka majeshi zaidi ya serikali jimboni humo, kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya Poires.
Nuevo Laredo ndio kilikuwa kitovu cha vurugu kati ya makundi ya Sinaloa na Gulf ambapo maelfu ya watu waliuawa mwaka 2003 na vurugu hizo kusambaa Mexico yote.
Mwaka huo, aliyekuwa kiongozi wa kundi la Gulf, Osiel Cardenas alikamatwa na kumshutumu kigogo wa dawa za kulevya, Joaquin 'El Chapo' Guzman, kuwa legelege, akijaribu kwenda Nuevo Laredo kusitisha mapambano hayo ya umwagaji damu.
Majumba makubwa ya kifahari na migahawa iligeuzwa kuwa kambi za kundi la Zetas, na wakati huo kufanya kazi ya kulisaidia kundi la Gulf, na kundi la Sinaola wakiendesha mapambano yao kwa kutumia bunduki na mabomu kutokea nje ya mji huo nyakati za mchana.
Mauaji ya rushwa katika polisi vilishamiri kiasi cha kwamba Rais wa wakati huo Vincente Fox alilazimika kupeleka mamia ya vikosi vya askari na mashushu, na mtu pekee aliyekuwa jasiri kuchukua nafasi ya Mkuu wa Polisi alipigwa risasi na kufa saa chache baada ya kuapishwa.
Kundi la Zetas lilishinda mapambano hayo na kutawala mji huo kwa mashaka, wakitisha polisi, waandishi wa habari na maofisa wa jiji na kupora fedha kutoka kwa wafanyabiashara.
Walivunja ndoa yao na kundi la Gulf mwaka 2010, huku wakichochea ghasia zaidi ukanda wote wa kaskazini-mashariki mwa Mexico.
Lakini mwezi uliopita, miili 14 iliyoharibiwa vibaya ilikutwa kwenye gari liliachwa katikati ya jiji.
Baadhi ya vyombo vya habari vimesema kundi la Sinaloa linahusika na miili hiyo yote na inadaiwa ujumbe ulisainiwa na kiongozi wao, Guzman, akisema kundi hilo limerejea Nuevo Laredo 'kusafisha' jiji.
Zaidi ya watu 50,000 wameuawa tangu serikali ya Mexico ilipoanza kampeni kabambe kukagua na kudhibiti usafirishaji dawa za kulevya mwaka 2006.

No comments: