1: Mama wa muuaji William, Michelle Davis-Balfour (katikati) akijificha uso baada ya mwanae kutiwa hatiani kwa mauaji ya watu watatu. 2: Marehemu Jason Hudson. 3: Marehemu Julian King. 4: Jumba ambamo mauaji yalifanyika ya mama yake Jennifer sebuleni na kaka yake chumbani. 5: Jennifer Hudson (kushoto) na dada yake kipenzi, Julia wakiwa na marehemu mama yao, Darnell Donerson (katikati). 6: Jennifer Hudson. 7: William Balfour.
Katika hali ya kibinadamu Jennifer Hudson ameanza maombi kwa ajili ya mtu aliyepatikana na hatia ya mauaji ya mama yake mzazi, kaka yake na mtoto wa dada yake.Mwimbaji huyo ambaye ni mshindi wa Tuzo za Academy na mwigizaji ameandika kwenye waraka wake Ijumaa jioni kwamba 'Mungu atamsamehe William kutokana na matendo aliyofanya na kubadili moyo wake siku moja.'
Yeye na dada yake, Julia wamemshukuru Mungu, wanasheria wao na mamlaka zilizohusika kwenye kesi hiyo, na wote waliokuwa wakifuatilia mashitaka hayo duniani kote ambao wamewapa nguvu.
Waliandika: 'Tumehisi upendo na msaada kutoka kwa watu duniani kote na tunashukuru sana kwa hilo. Familia ya Hudson tunaiombea familia ya Balfour. Wote tumeathirika kwa kupoteza wapendwa wetu katika janga hili.'
Madada hao walihitimisha: 'Ni maombi yetu kwamba Mungu atamsamehe William kwa haya aliyofanya na siku moja atambadili moyo wake.'
Shemeji huyo wa zamani wa Jennifer amekutwa na hatia ya mauaji ya mama, kaka na mtoto wa dada yake mwenye miaka saba katika kile waendesha mashitaka wamekiita malipizi kutoka kwa mume aliyeathirika kisaikolojia.
Baraza la Wazee wa mahakama lilimtia hatiani William mwenye miaka 31 katika mashitaka matatu Ijumaa, baada ya siku tatu za kusikiliza shauri hilo.
William anakabiliwa na kifungo cha maisha jela.
Jennifer alikuwapo mahakamani hapo, na alionekana akifuta machozi taratibu wakati shauri hilo likisomwa, na kisha baada ye alionekana na dada yake wakitabasamu.
Wakati William hakuonesha hisia zozote usoni wakati akisomewa mashitaka yake, watu wa familia yake walikuwa wakilia mahakamani hapo.
Mwanasheria wa William, Amy Thompson amesema kwamba bado anaandaa utetezi zaidi kwa ajili ya kuwasilisha mahakamani Juni huku akiamini kwa kusema 'kuna matumaini.'
Wakati huohuo Mwanasheria wa Serikali wa Cook County, Anita Alvarez amelishukuru baraza huku akiwaita wauaji kama 'viumbe wenye damu baridi na wasiokuwa na utu.'
Baraza hilo liliundwa na wanaume sita na wanawake sita.
Jennifer alikuwa shahidi wa kwanza kuitwa mahakamani na amekuwa akihudhuria kila siku ya kusikilizwa shauri hilo.
Katika dakika 30 ambazo waliziita mashahidi wawili tu, hata hivyo hawakuweza kutoa vidhibiti kusaidia ushahidi wao wa maneno.
Jennifer Hudson ambaye alikuwa mjini Florida wakati wa mauaji hayo, alihudhuria kila siku katika usikilizwaji wa shauri kwa wiki zote mbili akionekana mtulivu wakati picha za miili ya ndugu zake wakionekana wametapakaa damu zikipitishwa kwa wazee wa baraza wakati wa kufunga mjadala.
Akifahamika kwa kuvaa nguo za wabunifu kwenye zulia jekundu la Hollywood, Jennifer alivalia nguo zote nyeusi siku ya mashitaka.
Jennifer mwenye miaka 30 umaarufu wake ulianza mwaka 2004 pale alipoibuka kidedea kwenye Fainali za American Idol.
Katika ushahidi wake alielezea kumfahamu William miaka kadhaa iliyopita lakini wakati wote alikuwa akimchukia mno.
William alikuwa akiishi kwenye nyumba ya Jennifer yenye vyumba vitatu vya kulala iliyoko Englewood baada ya kumuoa Julia mwaka 2006.
Aliondoka hapo mwaka 2008 baada ya kutofautiana na mkewe, lakini mashahidi wamewaeleza wazee wa baraza kwamba alikuwa akilazimisha kurudi nyumbani hapo.
Mauaji hayo yalitokea asubuhi baada ya sherehe ya kuzaliwa Julia, na waendesha mashitaka wamesema William alikasirika mno baada ya kukuta zawadi maputo nyumbani hapo kutoka kwa rafiki mpya wa kiume wa Julia.
Baada ya mkewe huyo waliyetengana naye ambaye ni dereva wa basi kwenda kazini asubuhi ya Oktoba 24, 2008, waendesha mashitaka wamesema William alirejea nyumbani hapo akiwa na bunduki na kumfyatulia risasi mgongoni mama yake Jennifer, Darnell Donerson mwenye miaka 57.
Kisha akamfyatulia risasi mbili kichwani Jason mwenye miaka 29 aliyekuwa amejilaza kitandani.
Waendesha mashitaka wamesema William baadaye akatoweka nyumbani hapo kwa kutumia gari la Jason akiwa amemchukua Julian ambaye ni mtoto wa Julia ambaye amekuwa akimwita Boksi la Juisi na kumpiga risasi mvulana huyo mara kadhaa kichwani akiwa amejilaza kwenye kiti cha nyuma.
Mwili wa Julian ulikutwa ndani ya gari lililotelekezwa maili kadhaa kutoka hapo baada ya msako mkali wa siku tatu.
Upande wa utetezi ulijaribu kujenga picha kuwa William ni mume aliyekasirishwa kwa kusema walikuwa wakiendelea kufanya mapenzi na Julia hadi siku chache kabla ya mauaji hayo.
Waendesha mashitaka wamesema alifanya mauaji ya watu watatu kwa wivu baada ya mkewe waliyetengana kukataa ombi lake la kurudiana naye.

No comments:
Post a Comment