Kinyago cheusi kinachofunika uso ambacho Michael Jackson anadaiwa kuvaa siku moja kabla ya kufikwa na mauti mwaka 2009, kimevunja rekodi ya mauzo katika mnada ambapo bei imevuka Dola za Marekani 20,000.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa madalali wa kampuni ya udalali ya Nate D. Sanders, Michael Jackson alivaa kinyago hicho wakati wa mazoezi kujiandaa kwa ziara yake ya tamasha la 'This Is It' Juni 24, mwaka 2009, yakiwa ni mazoezi ya mwisho kabisa ya mwimbaji huyo.
Madalali hao walidai kinyago hicho kimetengenezwa kwa nyuzi ya hariri ikiwa ni ubunifu wa Mfalme huyo wa Pop duniani, likiwa na matundu kwa ajili ya kuonesha vipodozi anavyopaka Michael anapokuwa jukwaani katika maonesho mbalimbali pamoja na nywele zake nyeusi.
Mmoja wa mabaunsa wa zamani wa Michael Jackson ndiye alikuwa akilimiliki kinyago hicho. Mfalme huyo wa Pop alikuwa akivaa kinyago hicho wakati wa matembezi yake kama moja ya njia za kuepuka usumbufu njiani.
Mnada huo unafungwa rasmi Aprili 30 na zabuni zimeshafikia bei ya Dola za Marekani 21,190. Madalali wanakadiria kinyago hicho kitauzwa kati ya Dola za Marekani 50,000 na 150,000.

No comments:
Post a Comment