Nilikuwa nasafari kwa ndege kutoka Dar es Salaam kwenda Kampala. Wakati tukijiandaa kuondoka tulilazimika kuchelewa kwa dakika 45 na kila mmoja alikereka kwa hilo. Bila kutarajia tukatua Mwanza tukiwa njiani. Mhudumu wa ndege akatutangazia tutakaa hapo kwa dakika nyingine 45 na kama tukipenda tunaweza kuzurura nje kwa dakika 30 kabla ya kurejea na kuendelea na safari. Kila mtu akatoka nje isipokuwa jamaa mmoja ambaye alikuwa kipofu. Nilimgundua wakati nikipita na nikajua kuwa si mgeni kupanda ndege ile kwa jinsi mbwa wake alivyokuwa ametulia chini ya kiti. Mara rubani akamfuata na kumuita yule kipofu kwa jina, "Ssebo, tumetua kidogo Mwanza. Je, ungependa kunyoosha miguu nje?" Ssebo akajibu, "Hapana, labda umchukue mbwa wangu akatembee kidogo nje." Ile kutoka tu yule rubani huku akiwa ameshikilia mkanda wa mbwa, abiria wote wakapatwa na kigugumizi. Mbaya zaidi siku hiyo rubani alivaa miwani myeusi. Kila mtu akajua tunaongozwa na rubani kipofu, unaambiwa zikaanza pilika za kuhangaika kutafuta tiketi za ndege nyingine, yaani ni vurugu mtindo mmoja! Duh, mambo mengine bwana...
No comments:
Post a Comment