Thursday, April 19, 2012

ANUSURIKA KUKATWA MKONO BAADA YA KUNG'ATWA NA BUIBUI...

Kwa yeyote anayeogopa buibui, na mmoja akakwea kitandani kwako na kukung'ata hakika ni kitu kama vile unaota.
Lakini kwa Catherine Coombs, ndoto hiyo bado imeendelea kwa takribani miezi miwili zaidi, wakati jeraha la kung'atwa na buibui anayesadikika kuwa hatari mwenye sumu kali nchini Uingereza, nusura limsababishie apoteze mkono wake wa kushoto.
Mwanamke huyo mwenye miaka 48 aliamka huku akisikia maumivu makali usiku mmoja mwezi Februari, na mkono wake ukaanza kuvimba kwa kasi ya ajabu.
Alikimbizwa hospitali ambako madaktari walimfanyia upasuaji mara tatu kuondoa sumu na kutibu nyama katika harakati za kujaribu kuepusha madhara kusambaa kwenye mkono wote.
Ilifika wakati hali yake ikabadilika na kuwa mbaya kiasi cha madaktari kuhofia kwamba watalazimika kukata mkono wake.
Joto lake la mwili lilipanda sana na ngozi yake kuanza kubadilika na kusababisha madhara kwenye mmoja wa mguu wake wakati dalili za sumu kusambaa kupitia mfumo wake wa damu zikiongezeka.
Catherine alikaa hospitalini kwa wiki sita na sasa yuko nyumbani akisubiria madhara kwenye mwili wake yatoweke kabisa kabla ya kurejea hisia kwenye mkono wake huo ambao kwa sasa umepooza.
Kutokana na alama ya kwenye mkono na dalili alizokuwa nazo Catherine, ni wazi kwamba buibui huyo anafanana na aina ya buibui weusi.
Catherine, mpigapicha wa zamani anayeishi jirani na Poole, Dorset, alisema: "Nimekuwa nikiogopa sana buibui katika maisha yangu.
"Watu wamekuwa wakisema ni tabia ya kipuuzi na kwamba hawezi kukudhuru, lakini sasa nimejua wanaweza kukudhuru."
Aliongeza: "Kwa kipindi kirefu madaktari walikuwa wakihofia kuwa nitapoteza mkono wangu kabisa na nilikuwa nikisaini mara kwa mara kwa ajili ya zoezi la kukatwa mkono kila nilipoenda kwa matibabu.'
"Kila mara madaktari wakifanya upasuaji waligundua madhara zaidi na zaidi. Walikuwa wakiendelea kukata na kuondoa nyama iliyoharibika mkononi. Kila nilipoamka nilihakikisha mkono wangu bado upo."
Aliendelea: "Kwa wiki ya kwanza nilijisikia mnyonge na joto lilikuwa juu sana na ilikuwa kama dalili za mafua makali.
"Maumivu kwenye mkono wangu yalikuwa makali mno na walinifanyia upasuaji mara tatu ndani ya siku saba au nane.
"Wakati huo ilionekana kama siwezi kupona. Niliamini kabisa kuwa ningekufa kama ingeshindikana kutibika. Sumu kali ya buibui huyo ikiendelea kutapakaa ni hatari sana na hakuna swali kwanini isitibike.
Amewatahadharisha wengine kujilinda na hasa watoto wadogo wanapocheza nje ni rahisi kushika buibui.
Buibui hao weusi huwa na uzito unaofikia gramu 50 lakini wana aina ya kipekee ya ung'ataji tofauti na aina nyingine ya buibui katika Uingereza.
Wamekuwa wakionekana zaidi kusini mwa Uingereza japo sasa inaaminika wamezagaa nchi nzima kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Wengi wao, wanang'ata pale tu wanapochokozwa, na Catherine anaamini alichangia hilo pale alipokuwa akijaribu kujigeuza kitandani wakati amelala.
Mwezi Februari, Baba wa mtoto mmoja Chris Galton mwenye miaka 31 aliangua baada ya kung'atwa mgongoni na shingoni mara kumi na buibui wa aina hiyo mjini Southampton.

No comments: