Friday, April 20, 2012

ALIYEKARIBIA KIFO MARA MBILI, AGEUKA TEGEMEO KATIKA OLIMPIKI


Msichana mmoja ambaye mara mbili alichungulia kaburi ameweka kando matatizo hayo yaliyomkuta awali na kuibuka kuwa tmaini jipya la Uingereza kwenye Michezo ya Olimpiki.

Monique Newton mwenye miaka 19, aliugua kansa ya ubongo wakati wa utotoni, na kisha kujaribu kujiua kwa kumeza vidonge wakati alipotimiza miaka 15.
Sasa mwanamichezo huyo mzaliwa wa jijini London ameushinda udhaifu aliokuwa nao na kuwa bingwa wa dunia wa kuinua uzito huku akijifua vilivyo kupata mafanikio kwenye Michezo ijayo ya Olimpiki wakati majira ya joto.
Akiwa na uzito wa kilo 48 tu, msichana huyo mrembo, ambaye kwa sasa amekuwa akionekana kwenye mabango makubwa katika sehemu ya kampeni ya adidas ya "London -Chukua Hatua', anaweza kunyanyua uzito unaofikia mara tatu ya uzito wa mwili wake kupita kichwa.
Monique anayetokea mjini Fulham, aliugua maradhi hayo akiwa na miaka mitatu. Ugonjwa huo ulifikia hatua ya nne, ambayo ni ya hatari zaidi na familia yake ilitaarifiwa kuwa ataishia kutembea kwa kutumia kiti cha magurudumu ndani ya kipindi cha mwaka mmoja unaofuata na kwamba angefariki ndani ya kipindi cha miaka miwili.
Miezi ya kusikilizia maradhi yake hayo ilifuatia, na kushinda mabaya yote, Monique akaepuka kifo.
Lakini baada ya kupigania afya yake, mapambano ya Monique hayakuisha. Akiwa kijana, aliangukia mikononi mwa marafiki wabaya na kujikuta katika malumbano na wazazi wake, kisha akatoroka nyumbani akiwa na miaka 15 tu.
Akisumbuliwa na msongo wa mawazo na kutengwa na familia yake, Monique akabwia vidonge kibao aina ya paracetamol kwa lengo la kujiua.
Bahati aligundulika mapema na kukimbizwa hospitali na kutapishwa sumu ya dawa hiyo kutoka tumboni.
Baada ya kupambana na msongo wa mawazo uliokuwa ukimkabili, Monique alikwenda chuo na kupata kazi ya uhandisi.
Maisha yake mapya yakampa nafasi ya kuanza kunyanyua uzito na kujigundua kuwa ni mwanamichezo wa kiwango cha juu.
"Nimechagua kunyanyua uzito sababu nilitaka kufanya kitu ambacho nitaanzia chini kabisa na kujituma hadi kufikia ngazi ya juu," alisema.
Monique sasa ameshinda mara mbili ubingwa wa Uingereza na Dunia katika kunyanyua uzito, huku akishinda mara 18 kati ya 19 katika michuano aliyoshiriki hadi sasa, ikiwa ni pamoja na ubingwa wa michuano ya dunia kwa mara ya pili iliyofanyika nchini Latvia.
Japokuwa sasa anapigania kuwa fiti, Monique anasema familia yake inamtazama kama msichana mwenye afya mgogoro. "Siku moja nilipokuwa nikimsaidia shangazi yangu kubeba manunuzi sokoni, hakutaka kabisa nibebe mifuko kadhaa - alidhani itakuwa mizito mno kwangu kuweza kuibeba."
"Inanifanya nijisikie furaha kujua naweza kutumia historia yangu kusaidia watu wengine ambao na watakaopitia historia kama yangu," amesema.
"Sasa nakumbuka zamani. Nina furaha sana. Bado nipo hai leo," alimalizia.

No comments: